NI takribani mwaka mmoja sasa, tangu serikali ilipotangaza vipaumbele vipya kwenye elimu kwa vya kutoa mikopo kwa wanafunzi wa stashahada.
Vipaumbele hivyo vimejikita katika maeneo sita ambayo yalitengewa Sh. bilioni 48 kuwakopesha wanafunzi 8,000 waliokuwa wafanyiwe udahili katika mwaka wa masomo 2023/24.
Mwaka wa masomo mpya wa 2024/25 unaanza na waombaji wanatarajia kuanza masomo wiki ijayo, na huu ndiyo wakati wa kuwakumbuka Watanzania hasa vijana wanaojikita katika taaluma tofauti zinazohusika na kozi za teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA).
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, Oktoba mwaka jana, anazindua ‘Mwongozo wa Utoaji Mikopo ya Elimu kwa Wanafunzi wa Stashahada’ kwenye ofisi ndogo za Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Dar es Salaam.
Anasema uamuzi huo ni marekebisho ya sheria ya HESLB ya mwaka 2017 wa kuwahusisha wanafunzi wa ngazi hiyo.
Aidha, anasema ni mara ya kwanza kwa Tanzania kutoa mikopo kwa wanafunzi wa ngazi ya stashahada.
Kwa maendeleo ya taaluma ni hatua njema. Lakini, ikumbukwe huo ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan, kutaka wanafunzi wa vyuo vya kati kunufaika na mikopo ya serikali.
Anasema kinachofanyika ni utekelezaji wa maazimio ya Afrika kuhusu kuendeleza rasilimali watu.
Mikopo hiyo ipo katika vipaumbele sita na mahsusi kwa wanaosoma kozi za afya na sayansi shirikishi; elimu, zipo stashahada za ualimu wa fizikia, hisabati na amali.
Kadhalika kuna usafiri na usafirishaji, uhandisi wa nishati, madini na sayansi ya ardhi, kilimo na mifugo.
Mbali na vipaumbele hivyo, ni wazi serikali imesahau eneo muhimu kulipatia mikopo nalo ni stashahada ya TEHAMA ambayo ndio msingi na tegemeo kubwa kwenye sekta zote za maendeleo kuanzia afya, kilimo, mifugo, fedha, maji, elimu, nishati na madini.
Hivi sasa ubunifu na uandaaji wa shughuli za maendeleo unawategemea wataalamu wa TEHAMA ambao ndiyo wabobezi wa mifumo na mbinu tofauti na kutoa tafsiri za mambo ya kufanya na jinsi ya kuyafanikisha kielektroniki.
Kadhalika, katika sekta ya afya kipaumbele kimojawapo cha kupatiwa mkopo huo, asilimia karibu 70 ya kazi zake zinafanyika kwa kutegemea teknolojia.
Ni kazi zote za matibabu kwenye hospitali kuu na kwenye vituo vya afya ambako, wanahitajika wataalamu wa TEHAMA kama ilivyo viwandani na kwenye usafirishaji.
Vifaa vilivyoko hospitalini vingi ni vya kidijitali kuanzia X-ray, CT Scan, MRI, Ultra sound na hata vipimo vidogo enzi za kutumia muda mrefu kusubiri majibu ya vipimo kwa magonjwa maabara umepitwa na wakati, kutokana na kukua kwa teknolojia.
Kadhalika, hivi sasa uandikishaji wa wagonjwa kuanzia ngazi ya chini hadi rufani, hutegemea TEHAMA na si ile mfumo wa majalada uliokuwa unapoteza taarifa kwa vile kila wakati mafaili yalinyofoka leo kila kitu kinatunza mtandaoni.
Kadhalika taarifa zinamfikia daktari kupitia kompyuta ofisini kwake moja kwa moja linapokuja suala la mgonjwa fulani anayemhudumia.
Matibabu hutumia tiba mtandao, kuna aina kadhaa za upasuaji na upangaji wa dawa kwa wafamasia wakitegemea teknolojia ya kompyuta kwa kutunza kumbukumbu kujua iwapo dawa fulani ipo stoo au la, na inaweza kupatikana wapi, si kama awali ilihitaji mtu azame stoo kupekua, ndipo ajue idadi ya dawa zilizopo.
Madaktari bingwa miaka hii wanabadilishana uzoefu na wenzao walioko nje na ndani ya nchi kwa njia ya TEHAMA wakiunganisha mawasiliano ya video na wenzao popote duniani, kumfanyia upasuaji mgonjwa bila kuhitaji kumsafirisha au bingwa kusafiri na kumfikia kwa huduma.
Hembu fikiria, hivi sasa kwa kutumia programu tumishi (application), mtandaoni huduma ya M-mama, imeleta faraja miongoni mwa wajawazito na wazazi kwa kuokoa mamia ya wanawake na vifo vyao kupungua.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED