CAF itoe adhabu ya kuziondoa mashindanoni timu zenye fujo

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:43 AM Sep 23 2024
Ligi ya Mabingwa Afrika
Picha:Mtandao
Ligi ya Mabingwa Afrika

IMEANZA kuwa ni kawaida sasa kwa timu kufanyiana fujo kwenye michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Kwa miaka ya hivi karibuni, mchezo ule wa timu za Afrika Kaskazini kuzifanyia fujo timu zinazokwenda kucheza michezo ya kimataifa kwao imeanza kurejea tena.

Miaka ya 1960 hadi 1970, mpaka 1990 ilikuwapo, lakini baada ya kupewa adhabu ikiwamo mashabiki wao kufungiwa kutoingia viwanjani, na wakati mwingine timu zao kutoruhusiwa kucheza nchini kwao, na hata kutolewa kwenye michuano ilizaa matunda na klabu hizo kuanza kuwa na nidhamu.

Cha kushangaza kwa miaka ya karibuni umeanza kuzuka mchezo huu, ambayo si wa kiungwana hata kidogo katika kile ambacho FIFA wanakiita 'fair play'.

Mfano tuliona wachezaji wa Simba na baadhi ya viongozi wao walivyofanyiwa katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika, kwenye Uwanja wa Juni 11 jijini Tripoli, ilipocheza dhidi ya Al Ahli Tripoli nchini Libya.

Kulizuka vurugu kubwa, ambapo kwa mujibu wa Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, alisema wachezaji wao walianza kufanyiwa fujo na mashabiki, kabla ya mchezo na hata mchezo ulivyokuwa unaendelea hasa kule pembeni wakati wa kwenda kurusha mpira au kupiga kona, walikuwa wakirusha makopo na chupa za plastiki.

Kasheshe ilikuwa kubwa pale mechi ilipomalizika na mashabiki kushindwa kupata kile walichotarajia kutoka kwa timu yao, ilipotoka suluhu.

Ilibidi wanausalama kuwakimbiza wachezaji wa Simba vyumbani, lakini katika namna ya kushangaza, kule jukwaani nako baadhi ya viongozi walifanyiwa fujo, huku ikidaiwa mwanausalama mmoja akimpiga Aishi Manula aliyekuwa amekaa jukwaani.

Hata hivyo, tayari Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Patrice Motsepe, ameagiza kufanyika uchunguzi dhidi ya vurugu hizo.

Klabu ya Simba nayo ikaamua kutuma mlalamiko CAF dhidi ya Al Ahli Tripoli juu ya kurushiwa chupa za maji za plastiki, lugha mbaya, matusi, maneno ya kibaguzi na kushambuliwa kwa wachezaji na baadhi ya viongozi wa timu hiyo.

Wakati hayo yakiendelea kulizuka vurumai kubwa juzi katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya MC Alger ya Algeria na US Monastir ya Tunisia.

Kwenye mchezo wa marudiano uliochezwa nchini Algeria, MC Alger ilishinda mabao 2-0 na kutinga makundi kwa jumla ya mabao 2-1, kwani katika mchezo wa kwanza ilipoteza nchini Tunisia kwa bao 1-0.

Kulizuka tafrani kubwa kuanzia uwanjani, mpaka kwenye vyumba vya kuvalia. Mimi naona umefika wakati kwa CAF kuziondoa mashindanoni timu zote ambazo mashabiki wake wanafanya fujo, au viongozi kuwafanyia vurugu wageni wao.

Hii nadhani inaweza kuwatia woga kuliko kuzipiga faini kwani inaonekana wala hazihofii chochote na wanaweza kufanya lolote kwa sababu faini ya fedha kwao si tatizo kulipa.

Ikumbukwe timu zinazofanya hivi nyingi ni za Afrika Kaskazini, ambazo ziko vizuri sana kiuchumi, hivyo zinajua zitafanya fujo kwa maslahi ya timu zao na zitalipa faini.

Hebu angalia, baada ya kuona kuwa imewafanyia fujo Simba, yenyewe Al Ahli Tripoli ikajihami kwa kukodisha mabaunsa ilipokuja nchini kwenye mechi ya marudiano.

Imefika wakati sasa CAF kuchukua hatua ya kuzipa adhabu kali klabu za aina hii kwani kuziacha ni kuonekana kama inaziogopa. Na tabia hii ikiendelea ipo siku yatatokea maafa makubwa uwanjani. CAF isisubiri majeruhi au vifo ili ichukue hatua.