Yanga yaandaa ‘surprise’ sherehe za ubingwa Bara

By Saada Akida , Nipashe
Published at 08:57 AM May 21 2024
Ofisa habari wa klabu hiyo, Ali Kamwe.
Picha: Yanga SC.
Ofisa habari wa klabu hiyo, Ali Kamwe.

MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga wameandaa ‘surprise’ kwa mashabiki wao wakati wa sherehe za kukabidhiwa kombe la ubingwa huo, Mei 25 jijini Dar es Salaam.

Kikosi cha Yanga kimerejea jana kutoka Arusha, leo wanaelekea Dodoma kwa ajili ya mchezo dhidi ya Dodoma Jiji FC kabla ya kurejea Dar es Salaam kukabiliana na Tabora United. Akizungumza na Nipashe jana, ofisa habari wa klabu hiyo, Ali Kamwe, alisema siku hiyo ya mechi dhidi  ya Tabora United itakuwa na mambo mengi mazuri kwa ajili ya mashabiki wao na watafanyia ‘surprise’ kubwa Wanayanga kabla ya kuanza kwa mchezo huo saa 10:00 jioni.

Alisema mchezo dhidi ya Dodoma FC utakuwa maalum kulishukuru benchi la ufundi kwa kazi nzuri na wameipa jina siku hiyo na kuiita ‘Gamondi Day’. 

“Katika mchezo huu, ikifika dakika ya 30 mashabiki tutawaomba wasimame  na kupiga makofi kulipongeza benchi letu la ufundi kwa kufanikisha ubingwa wetu wa 30.

“Alhamisi tunaenda bungeni  baada ya kupata mwaliko kutoka Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo kusikiliza hotuba za bajeti zinazoendelea, baada ya hapo  tunarejea Dar es Salaam  kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa Mei 25, tumeomba mechi hii tukabidhiwe kombe letu la ubingwa,” alisema Kamwe. 

Alisema siku ya kukabidhiwa kombe lao itakuwa siku ndefu yenye furaha ambapo mashabiki watatamba na kuvimba kwa sababu ni siku ya mabingwa. 

Aliongeza kuwa wamepeleka maombi serikalini na Bodi ya Ligi kuomba kuutumia Uwanja wa Benjamin Mkapa kucheza mchezo huo na kukabidhiwa kombe lao. 

 “Siku hiyo tutakuwa na burudani mbalimbali, tayari tiketi zimeanza kuuzwa, baada ya utaratibu wa mchezo kumalizika shughuli za sherehe zitaendelea hadi asubuhi,” alisema Kamwe. 

“Tumepanga kuondoka uwanjani hapo Jumapili Mei 26 na kulipeleka kombe letu makao makuu ya klabu, tutatumia njia ya Temeke mpaka Kariakoo, tukifika pale Msimbazi tutasimama kidogo na baadaye kuendelea na safari mpaka klabuni kwetu,” alisema Kamwe.