Timu za Majeshi zatakiwa kupigania michuano CAF

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:56 AM Jul 22 2024
Nembo ya CAF.
Picha: Mtandao
Nembo ya CAF.

TIMU za Majeshi zimetakiwa kufanya usajili mzuri wa wachezaji ili ziweze kushiriki mashindano ya kimataifa kama zinavyofanya Simba, Yanga pamoja na Azam FC.

Hayo yalisemwa juzi jioni na Meja Jenerali, Maiko Jocob Muhona,  ambaye alimwakilisha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda, kwenye ufunguzi wa mashindano ya Mkuu wa Majeshi (CDF Cup 2024), yanayoendelea kwenye viwanja mbalimbali Dar es Salaam. 

"Tunatamani kuona timu za majeshi zinashika nafasi za juu na kupata fursa ya kushiriki mashindano mbalimbali ya kimataifa kama zilivyo Simba, Yanga na Azam FC," alisema.

Alisema lengo la mashindano hayo ni kuadhimisha Miaka 60 ya Jeshi la Ulinzi na kudai yatasaidia kuunda timu itakayoshiriki katika mashindano ya timu za Majeshi (Bamata) Septemba, mwaka huu, mkoani Morogoro. 

Aidha, alimpongeza Mkuu wa Majeshi kwa kuamua kuyarudisha baada ya kutofanyika kwa kipindi cha miaka miatano, na kuwataka waamuzi watendeke haki katika michezo yao ili kuepusha malalamiko ya hapa na pale. 

Pia aliwataka vijana washiriki michezo kwani inajenga afya pamoja na kuwasaidia kupata ajira kwa urahisi. 

Wakati huo huo, Brigedia Jenerali Said Hamis Saidi, alisema mashindano hayo yameshirikisha Kamandi mbalimbali za jeshi ikiwamo nchi kavu, majini, anga pamoja na ile ya akiba.

"Kutakuwa na michezo mbalimbali itakayoshirikisha wanaume na wanawake ukiwamo mpira wa miguu riadha netiboli na kulenga shabaha, alisema Jenerali Saidi. 

Vilevile alisema mwaka huu wameongeza mchezo wa ngumi na kurusha mpito wakiwa na malengo ya kupata wachezaji watakaokidhi vigezo vya kwenda kushiriki mashindano ya Olimpiki ifikapo mwaka 2028 nchini Marekani.