Simba yaitisha KenGold

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:57 AM Dec 18 2024
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids
PIcha: Mtandao
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids

BAADA ya kumaliza majukumu ya mashindano ya kimataifa, Simba inatarajia kukutana na KenGold ikitamba haitakuwa na huruma katika mechi hiyo ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

Akizungumza jijini jana, Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, alisema watashuka kwa heshima na kamwe hawatawadharau KenGold kwa sababu inaburuza mkia katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara. 

Fadlu alisema wanakwenda kukabiliana na timu hiyo wakifahamu wametoka kupoteza mechi iliyopita waliyocheza na  Namungo licha ya wao kuanza kuongeza kwa mabao 2-0.

"Tunakwenda kucheza dhidi ya KenGold, ni timu iliyotoka kupoteza kwa kufungwa mabao 3-2 dhidi ya Namungo, lakini ikiwa imetangulia kwa kufunga mabao 2-0, tumeichunguza na kujua inacheza vipi na taarifa nyingine ambazo zinabaki mikononi wetu, lakini kifupi wanazuia zaidi na kushambulia kwa kushtukiza wakiwa na mawinga wao katika mbio, tumeliona hilo, sisi tunasema hatutaidharau timu hiyo, ila hatutaionea huruma," alisema kocha huyo raia wa Afrika Kusini.

Mara ya mwisho Simba kucheza mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara ilikuwa Novemba 22, mwaka huu ikiwafunga Pamba Jiji bao  1-0 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini, Mwanza, bao la penalti lililofungwa na Leonel Ateba.

Inakwenda kucheza mchezo huo, siku tatu tu baada ya kumaliza kucheza mechi ya raundi ya tatu ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, hatua ya makundi dhidi ya CS Sfaxien kutoka Tunisia, Mnyama akishinda mabao 2-1, mechi ikipigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Awesu Awesu, aliliambia gazeti hili wachezaji wote wamejipanga kuhakikisha wanapata ushindi na hawaidharau hata chembe KenGold, kwa sababu timu zote za Ligi Kuu hupania zaidi zinapocheza nao hata kama ipo chini katika msimamo wa ligi hiyo.

"Kila mechi ambayo Simba inacheza ni fainali, haijalishi KenGold ipo nafasi ya ngapi, hatujawahi kudharau mechi yoyote, na hii timu wala siyo timu mbovu kama inavyosemwa, ni matokeo tu, sisi wachezaji tumejiandaa vizuri sana tuna imani mchezo utakuwa bora na tutashinda," alisema Awesu aliyesajiliwa msimu huu akitokea KMC.

Naye Kocha Mkuu wa KenGold, Omari Kapilima, alisema timu yake imejiandaa vyema kukabiliana na Simba katika  mchezo huo wanaotarajia utakuwa mgumu.

"Tumejiandaa vizuri, Simba ni timu kubwa, ina benchi bora la ufundi na wachezaji wa kiwango cha hali ya juu, lakini na sisi tumejiandaa kukabiliana nao," Kapilima alisema.

Aliongeza amewataka wachezaji wake kuongeza utulivu katika mchezo huo na anaamini wakiwa makini wanaweza kuondoka na pointi tatu.

Kwa sasa Simba iko katika nafasi ya tatu ya kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 28 baada ya kucheza michezo 11 wakati KenGold iliyoshuka dimbani michezo 14 inaburuza mkia ikiwa na pointi sita kibindoni.

KenGold imeshinda mchezo mmoja, sare tatu na imepoteza michezo 10.