Simba kukoleza vita nafasi ya pili Ligi Kuu

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 09:07 AM May 21 2024
Kocha wa Simba, Juma Mgunda.
Picha: Mtandaoni
Kocha wa Simba, Juma Mgunda.

KOCHA wa Simba, Juma Mgunda, amesema kuwa licha ya ugumu wa mchezo wa leo dhidi ya Geita Gold FC, bado malengo yao ni kuipata nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Simba kesho itakuwa mwenyeji wa Geita Gold FC kwenye uwanja wa Azam Complex katika mchezo wa mzunguko wa 28 huku ligi hiyo ikielekea ukingoni.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mgunda alisema wanaiheshimu Geita Gold kwa kuwa nao wana malengo yao kwenye mchezo huo lakini wamejiandaa vizuri kuwakabili.

“Geita ni timu nzuri, bila kuangalia wapo katika nafasi ya ngapi, najua watapambana kutaka pointi tatu ndio sababu nasema hautakuwa mchezo mwepesi, pamoja na yote tumejiandaa vizuri kuwakabili,” alisema Mgunda.

Alisema kuwa ana matumaini ya kufanya vizuri na amewataka wachezaji wake kutowadharau wapinzani wao.

“Lakini kingine kikubwa, nawaomba mashabiki waje kwa wingi, shabiki ni mchezaji wa 12, siku zote ana nafasi yake kwenye ushindi wa timu, natarajia watajitokeza kesho (leo) kama ilivyo kawaida,” alisema Mgunda.

Simba inasaka kumaliza ligi katika nafasi ya pili ili kupata nafasi ya kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, nafasi hiyo wanachuana vikali na Azam FC ambao wote wanalingana kwa kuwa na pointi 60 baada ya kucheza michezo 27.