Serikali yakabidhiwa viwanja vipya

By Gwamaka Alipipi , Nipashe
Published at 10:36 AM Jul 26 2024
 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, Suleiman Serera.
Picha: TFF
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, Suleiman Serera.

SERIKALI imepokea msaada wa viwanja vitatu vya michezo vilivyojengwa katika Shule ya Msingi Kingolwira mkoani Morogoro.

Akipokea msaada huo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, Suleiman Serera alisema viwanja alivyokabidhiwa ni cha mpira wa miguu, mpira wa pete na mpira wa kikapu ambavyo vimejengwa na kampuni ya tumbaku ya Alliance One (AOTL) kwa gharama ya Shilingi milioni 241.

"Msaada huu unaenda sambamba na Sera ya Taifa ya Michezo ya Mwaka 1995 pamoja na maelekezo ya Rais Samia ya kufanya kazi kwa karibu na taasisi binafsi katika kuwaletea wananchi maendeleo," alisema.

Alisema msaada huo unaendana na mpango wa serikali wa kujenga miundombinu ya viwanja kwenye shule 56 nchini. Lengo likiwa ni kuweka mazingira bora ya michezo kwa watoto wa shule za msingi na sekondari.

Aidha, Serera aliishukuru kampuni hiyo kwa ujenzi wa viwanja hivyo ambavyo vitasaidia kuboresha mazingira yatakayosaidia kuibua vipaji vya watoto mashuleni.

Aidha, alisema viwanja hivyo vimejengwa kwa hadhi ya kimataifa na kwamba vimewekewa miundombinu ya maji ya umwagiliaji majani ili yasikauke.

"Niwapongeze sana Alliance One kwa ufadhili huu kwani natambua kwamba ziko taasisi nyingi ambazo zinapata faida na zinafanya mambo mengi na hawarudishi fadhila ipasavyo kwa jamii kama ninyi mlivyofanya kwani kutoa ni moyo wala siyo utajiri," alisema.

Msemaji wa kampuni hiyo, John Magoti alisema wametoa msaada huo kupitia sera yao ya misaada kwa jamii.

Aliendelea kuelezea kuwa, gharama za ujenzi wa viwanja hivyo umegharimu Sh. milioni 241, fedha ambazo zimelipwa kwa mkandarasi mzawa ambaye amefanya kazi kwa wakati.

“Tumetoa msaada huu tunaoukabidhi leo lengo likiwa ni kuendeleza michezo kwa watoto kwani tunaamini kwamba baada ya masomo ya darasani, kuna umuhimu kwa watoto kuwajengea watoto afya ya akili kupitia michezo ya aina mbalimbali inayochezwa kwenye mazingira mazuri,” alisema.

Akipokea msaada huo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Emmanuel Mkongo, aliipongeza kampuni hiyo kwa msaada wa viwanja hivyo huku akiahidi kuvitunza.

Aidha, Kaimu Mkurugenzi wa Aliance One, Blasius Lupenza alisema misaada wanayoitoa kwenye shule hiyo ni ya ujirani mwema na wamekuwa wakiifanya kwa miaka mingi.