TIMU ya Soka ya Taifa ya vijana ya umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys), inakutana na yosso wenzao wa Kenya katika mechi ya kusaka tiketi ya kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON U-17), itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Nakivubo jijini, Kampala nchini Uganda.
Katika mechi ya kwanza ya Kundi A, Serengeti Boys ilitoka sare ya bao 1-1 na wenyeji Uganda na leo inahitaji ushindi wowote ili kufuzu hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.
Kocha Mkuu wa Serengeti Boys, Aggrey Moris, alisema wachezaji wake wamejiandaa vyema kuelekea mchezo huo ambao ni muhimu ili kusonga mbele.
Moris alisema watashuka uwanjani kwa tahadhari kwa sababu wanafahamu Kenya pia itahitaji kupata matokeo chanya ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kucheza hatua inayofuata.
"Tunaenda kucheza mechi muhimu, tunajua Kenya pia inawachezaji wenye uwezo, tumewaandaa vijana kuongeza umakini na utulivu wanapokaribia katika lango la mpinzani, tumejipanga kupambana ili kupata ushindi na kujiweka katika nafasi nzuri," alisema kocha huyo.
Mechi nyingine ya mashindano hayo itakayochezwa leo ni kati ya Sudan Kusini dhidi ya Sudan.
Sudan Kusini watashuka dimbani wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 3-0 waliopata katika mechi ya kwanza ya Kundi B dhidi ya Somalia.
Fainali ya mashindano hayo yanayoshirikisha timu sita kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), itachezwa Desemba 27, mwaka huu.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED