Ngao ya Jamii hakutakuwa na dakika 120 - Bodi ya Ligi

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:50 AM Jul 23 2024
Ofisa Habari wa Bodi hiyo, Karim Boimanda.
Picha: Mtandao
Ofisa Habari wa Bodi hiyo, Karim Boimanda.

BODI ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB), imebainisha kuwa hakutokuwa na dakika za nyongeza kwa michezo yote itakayopigwa kwenye Ngao ya Jamii inayotarajiwa kuanza kupigwa Agosti 8, mwaka huu.

Ofisa Habari wa Bodi hiyo, Karim Boimanda, amesema mechi zote zitachezwa kwa dakika 90 na baada ya hapo ni mikwaju ya penalti itaamua mshindi.

Boimanda alisema hayo, alipokuwa akibainisha baadhi ya kanuni zitakazotumika kwenye michuano hiyo, pamoja na Ligi Kuu Tanzania Bara inayotarajiwa kuanza Agosti 16, mwaka huu.

Mbali na hayo, amesema wachezaji watakaotumika kwenye mechi hizo ni wale tu ambayo watakuwa wamekamilisha usajili wa kucheza Ligi Kuu na si vinginevyo kwani huko nyuma imeshawahi kutokea timu moja kuchezesha kwenye Ngao ya Jamii mchezaji ambaye baadaye ilibainika bado alikuwa hajakamilisha taratibu za kucheza ligi.

"Wachezaji wanaoruhusiwa kucheza Ngao ya Jamii ni wale ambao usajili wao umekamilika tu, ambao wameshasajiliwa kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa na hakutokuwa na dakika za nyongeza kwa mechi zote, kuanzia za nusu fainali, fainali hadi kusaka mshindi wa tatu, zikiisha dakika 90, zitapigiana mikwaju ya penalti," alisema Ofisa Habari huyo.

Agosti 13, 2022, Fiston Mayele alifunga mabao yote mawili, Yanga ikiichapa Simba 2-1 katika mechi ya Ngao ya Jamii, lakini baadaye iligundulika alikuwa hajakamilisha usajili kitu kilichosababisha kutocheza mechi za awali za Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huo.

Aliitaja kanuni nyingine ni kwamba, mchezaji yeyote ambaye alimaliza Ligi Kuu msimu uliopita akiwa na kadi nyekundu au adhabu ya kusimamishwa hata mechi moja kwa kuwa na kadi tatu za njano na hakuzitumikia kwa sababu ligi ilikuwa imemalizika, hatoruhusiwa kucheza kwani atatakiwa kutumikia adhabu yake.

"Kanuni hizi zinatumika pia kwenye Ligi Kuu. Kwa hiyo hata adhabu zinaingiliana, mchezaji mwenye kadi na hakutumikia hatatusubiri mpaka ligi hivyo atazitumikia kwenye Ngao ya Jamii. Lakini yeyote ambaye atapata kadi nyekundu kwenye michezo hiyo, ataitumikia pia kwenye michezo ya ligi," alisema.

Alisema wameamua kuanika baadhi ya kanuni hizo kutokana na mashabiki wengi kuwa na mkanganyiko hasa inapokuwa michezo kama hiyo ambayo ni ya mtoano, wasijue nini kinafuata baada ya timu kutoka suluhu.

Agosti 8, saa 10:00 jioni, Azam itakipiga dhidi ya Coastal Union, Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar. Na saa 1:00 usiku Simba itavaana na Yanga katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam na fainali ya Ngao ya Jamii itapigwa hapohapo Agosti 11, mwaka huu.