Meneja aonya watovu wa nidhamu Simba, ikizindua jezi mpya mbugani

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:43 AM Jul 25 2024
Patrick Rweyemamu
Picha: SIMBA SC
Patrick Rweyemamu

UONGOZI wa klabu ya Simba, umetangaza kumrejesha Patrick Rweyemamu kwenye nafasi ya Meneja wa timu hiyo, huku mwenyewe akisema amerejea kusimamia nidhamu ndani ya timu hiyo.

Rweyemamu aliwahi kushika nafasi hiyo ndani ya Simba kabla ya msimu uliopita kupelekwa kuwa kiongozi kwenye soka la vijana ndani ya Simba.

Rweyemamu ameteuliwa kuchukua nafasi ya aliyekuwa meneja wa timu hiyo, Mkenya Mikael Igendia.

Akizungumza akiwa Ismailia nchini Misri ambako alikwenda baada ya uteuzi, meneja huyo alisema kuna baadhi ya wachezaji huwa na dharau na mameneja kutokana na mishahara yao mikubwa, lakini yeye hufanya kila njia ili kurekebisha mambo.

"Mpira una vitu viwili au vitatu, kocha lazima aandaliwe mazingira rafiki ambayo ni nidhamu kwa wachezaji, kuna idara ya kitabibu, ukishaunganisha hivi vitu viwili ndiyo unakuwa umemrahisishia kocha kazi.

"Daktari atamwandaa mchezaji kimwili na kiakili, sisi mameneja nao lazima tumwandalie mazingira rafiki yaani kambi na nidhamu, bila hivyo huwezi kufanikisha kile ambacho unakitaka, vinginevyo kocha hawezi kupata kitu bora.

Nikisema nidhamu inajumuisha vitu vingi, kulala, kunywa, kula, starehe, mazoezi kwa hiyo inahitaji lazima Meneja uwe na Mamlaka, uwe na uamuzi mgumu unaoeleweka na usiopinda," alisema Rweyemamu.

Alisema kuna baadhi ya wachezaji ambao wanalipwa pesa nyingi lakini baadhi yao wanatumia hilo kudharau viongozi wao lakini kwake ni tofauti kwa kuwa atasimimamia nidhamu kwa kila mchezaji.

Wakati huo huo, klabu hiyo jana imezindua jezi zake za msimu ujao kwenye Hifadhi ya Wanyamapori mkoani Morogoro.

Viongozi wa klabu hiyo, wakiongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu, Imani Kajula, walionyesha jezi tatu za rangi nyekundu, nyeupe na bluu ambazo timu yao itazivaa kwenye mashindano mbalimbali pamoja na kuuzwa kwa mashabiki wake.

Jezi hizo zimezinduliwa wiki chache kabla ya kufanyika kwa tamasha la klabu hiyo maarufu 'Simba Day' ambalo litafanyika Agosti 3 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.