Meneja amkana Kibu Denis

By Faustine Feliciane ,, Shufaa Lyimo , Nipashe
Published at 10:31 AM Jul 25 2024
 Kibu Denis.
Picha: Mtandao
Kibu Denis.

SIKU moja baada ya uongozi wa Simba kutoa taarifa kwa umma juu ya utoro wa mchezaji wao, Kibu Denis, Meneja wa mchezaji huyo, Carlos Silyvester, ameibuka na kumkana mchezaji huyo kutokana na kile alichokifanya.

Akizungumza jana kwa njia ya simu, Carlos, amesema kuwa hafahamu mchezaji wake kwa nini ameshindwa kuungana na timu huku akiwa amelipwa pesa zake zote za usajili na kusaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia timu hiyo.

Alisema amesikitishwa na kitendo cha mchezaji wake huyo kuonyesha utovu wa nidhamu kwa waajiri wake hao.

"Kwa hilo la utovu wa nidhamu siwezi kuiingilia maamuzi yatakayofanywa na Klabu ya Simba, binafsi sipendi kuona mchezaji wangu anakuwa hana nidhamu kwa viongozi wake," alisema Silyvester. 

Meneja huyo aliweka wazi kuwa anachokifahamu mchezaji wake huyo alipata mwaliko kutoka Norway ambapo kuna timu inayoshiriki Ligi Kuu nchini humo inamhitaji. 

"Ninafahamu Kibu yupo Norway alipata mwaliko huo kutoka kwenye timu moja inayoshiriki Ligi Kuu nchini humo, masuala mengine siwezi kuyazungumzia zaidi ya hayo," alisema meneja huyo. 

Alisema sakata hilo limeanza baada ya mchezaji huyo kwenda mapumzikoni nchini Marekani.

Alisema yeye kama meneja wa mchezaji huyo anamtaka kukaa meza moja na uongozi wa Simba kama anataka kujiunga na timu hiyo ya Norway.

"Kibu anapaswa kufahamu, hakuna namna anaweza kuikwepa Simba kwani ana mkataba nao kama kuna jambo lolote ni vizuri kukaa mezani azungumze na viongozi wake kusudi jambo hili lifikie kikomo kabla timu haijarudi Dar es Salaam kutoka Misri," alisema.

Klabu ya Simba ilimwongezea mkataba wa miaka miwili nyota huyo ambao utafikia mwisho mwaka 2026 huku ikiwa imemlipa stahiki zake zote.

Katika taarifa ya Simba iliyotoka jana, imesema itamchukulia hatua za kinidhamu mchezaji huyo kwa utoro wake licha ya kutakiwa kuripoti kwenye kambi ya timu hiyo.

Kikosi cha Simba ambacho kipo Misri kwa zaidi ya wiki tatu sasa, kinatarajiwa kurejea nchini siku chache kabla ya kilele cha tamasha la 'Simba Day' litakalofanyika Agosti 3 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa