Kibu kikaangoni, Coastal ikilia na Simba kwa Lawi

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 09:29 AM Jul 24 2024
news
Picha: Simba SC
Denis Kibu.

WAKATI uongozi wa Klabu ya Simba ukisema haujui alipo kiungo mshambuliaji wao, Denis Kibu na hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake pindi atakaporejea, Klabu ya Coastal Union nayo imesema inawasubiri 'Wekundu wa Msimbazi' hao kukaa meza moja ili kulimaliza suala la beki Lameck Lawi.

Simba tayari wametimiza wiki tatu katika kambi yao kwenye mji wa Ismailia nchini Misri, lakini Kibu ni mmoja wa wachezaji ambaye hajaripoti kambini mpaka sasa.

Mchezaji mwingine ambaye hayupo kwenye kambi hiyo ni golikipa, Aishi Manula, ambaye bado yupo nchini.

Akizungumza na Nipashe jana, Msemaji wa klabu hiyo, Ahmed Ally, alisema uongozi wa klabu hiyo hauna taarifa ya wapi alipo Kibu na kwa sasa taratibu nyingine za ndani zinafanyika kumwadhibu mchezaji huyo.

"Hatujui wapi alipo, mara ya mwisho uongozi ulikuwa unafahamu amekwenda Kigoma mara moja baada ya kurudi kutoka mapumzikoni Marekani, lakini mpaka sasa hivi hatuna taarifa nyingine na hapatikani kwenye simu," alisema Ahmed.

Aidha, alisema kuwa zipo taratibu za ndani, Simba kama taasisi ambazo watazichukua juu ya mchezaji huyo.

"Simba ni taasisi kubwa ina mifumo yake, hili suala litafika kwa uongozi na watachukua hatua stahiki kwa mchezaji husika, ni kosa kutokuwapo kwenye kambi ya timu bila sababu," alisema Ahmed.

Katika hatua nyingine, Ahmed alisema golikipa Manula muda wowote kuanzia sasa ataungana na wachezaji wenzake katika kambi nchini Misri.

"Manula bado ni mchezaji wa Simba, na nakuhakikishia muda wowote kuanzia sasa ataungana na wenzake kambini kuendelea na maandalizi," alisema Ahmed bila kutoa ufafanuzi zaidi.

Kuhusu Lawi, Klabu ya Coastal Union imesema inausubiri uongozi wa Simba wakae meza moja kulimaliza pembeni sakata la usajili wa beki huyo.

Ikumbukwe baada ya Simba kupeleka malalamiko yao kwa Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), juu ya sakata hilo la usajili, klabu hizo zilitakiwa kukaa meza moja na kumalizana juu ya usajili wa mchezaji huyo ambaye Simba wanadai wamemsajili kihalali huku Coastal Union wakikana kwa kile wanachodai wenzao hao hawakufuata makubaliano yao.

Msemaji wa Coastal Union, Abbas El Sabri, alisema jana kuwa wao wanawasubiri mezani Simba kama walivyoshauri kamati hiyo ya TFF.

"Ni kweli tulipewa ushauri huo, sisi hatuna shida tunawasubiri wenzetu wa Simba watakapokuwa tayari tukutane kulimaliza suala hili, kama tulivyosema awali sisi hatua shida, Simba wakiwa tayari tutaenda kukutana nao," alisema El Sabri.

Hata hivyo, El Sabri alikiri licha ya mchezaji huyo kumworodhesha kwenye usajili wao msimu ujao, kwa sasa yupo nje ya nchi kwa mambo yake binafsi.

"Lawi yupo Ubelgiji kwa mambo yake binafsi, lakini ni mchezaji wa Coastal na tumepeleka jina lake CAF kwa ajili ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ambayo tutashiriki msimu ujao," alisema El Sabri.

Kwa upande wake, Msemaji wa Simba, Ahmed Ally, alisema kuwa suala hilo linashughulikiwa na uongozi wa juu wa klabu hiyo.

"Kama kutakuwa na lolote wana Simba watafahamu, kwa sasa suala hilo lipo ngazi ya juu na limefika TFF, mbivu na mbichi zitajulikana hapo pande zote zitakapokutana," alisema Ahmed.