UONGOZI wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga umesema endapo kipa, Khomeini Aboubakar, atakuwa na mwendelezo mzuri, wanaamini anafaa kuwa mrithi sahihi wa kipa wao namba moja wa sasa, Djigui Diarra, ambaye ni raia wa Mali, imeelezwa.
Khomeini aliingia katika mechi ya hatua ya makundi ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe iliyochezwa ugenini Mjini Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DR Congo) baada ya Diarra kuumia.
Kabla ya kuumia huko DR Congo, Diarra aliruhusu kufungwa bao 1-0 dhidi ya Azam FC na baadaye nyavu zake zikatikiswa tena Yanga ilipofungwa magoli 3-1 na Tabora United, mechi zote za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Diarra pia aliruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili walipocheza mechi ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal ya Sudan na alifungwa idadi kama hiyo ya mabao walipokutana ugenini na MC Alger kwenye michuano hiyo.
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alisema Khomein alionesha kiwango kizuri kwa dakika 45 za kipindi cha pili alizocheza katika mchezo huo uliochezwa Jumamosi iliyopita na kuongeza anaonekana atakuwa kuwa kipa wa kiwango cha juu nchini Tanzania.
Kamwe alisema baada ya kipa huyo kuchukua mikoba ya Diarra, viongozi walikuwa na wasiwasi na walipata mshangao kuona amefanya vyema muda wote aliokuwa langoni.
"Tunaamini kama atakuwa na mwendelezo ule tuliouona DR Congo, atakuja kuwa golikipa mzuri siyo kwa Yanga tu bali hata kwa taifa, unajua hakuna aliyeamini kama angeweza kudaka vile baada ya kuumia kwa Diarra, kila mmoja alikuwa na wasiwasi, lakini dakika 45 za pili alisimama imara langoni, hakuruhusu bao lolote," alisema Kamwe.
Katika mchezo huo, Diarra aliumia ingawa alijitahidi kuendelea na mchezo, lakini hakurejea tena uwanjani baada ya mapumziko na Khomeini, aliyesajiliwa mwanzoni mwa msimu huu akitokea Singida Black Stars akasimama langoni.
"Aliniambia ilikuwa ni mechi yake ya kwanza kimataifa na akasema ametimiza ndoto yake kwa sababu hakuamini kitu kama hicho kama anaweza kucheza mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, tena timu ikiwa ugenini, kwa hiyo amefurahi sana na imemwongezea kujiamini," Kamwe alisema.
Aliongeza pamoja na huenda akawa mrithi sahihi wa Diarra, lakini kwa sasa wanachama na mashabiki wa Yanga hawatakuwa na wasiwasi kama kipa huyo akiwa nje, kwa sababu kiwango alichowaonyesha katika mechi hiyo ya kimataifa kimempa nafasi ya kuanza kuaminika.
"Amecheza vizuri kwa kujiamini, sasa hata akiumia Diarra wanachama na mashabiki wa Yanga hawatakuwa tena na wasiwasi wa mtu atakayeshika nafasi yake, tumpongeze na tunaamini atakuwa na mwendelezo huo siku zote," aliongeza ofisa huyo.
Katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, Khomeini amedaka michezo miwili na yote alidaka dakika 90 bila kuruhusu bao.
Alidaka katika mchezo wa Yanga dhidi ya Coastal Union uliochezwa Oktoba 26, mwaka huu kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini, Arusha ambapo mabinga hao watetezi walishinda bao 1-0 na Novemba 30, mwaka huu timu yake ilipokuwa ugenini dhidi ya Namungo na kushinda mabao 2-0.
Wakati huo huo, kikosi cha Yanga kimeingia kambini mara baada ya kurejea nchini kutoka DR Congo, kwa ajili ya kujiandaa na mechi dhidi ya Mashujaa FC kutoka Kigoma itakayochezwa kesho
Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic, amesema atabadilisha mfumo aliocheza dhidi ya TP Mazembe, kutokana na kuona timu za Ligi Kuu Tanzania Bara zikikabia zaidi chini.
"Pia suala la utimamu wa mwili nimeshaanza kulifanyia kazi, nadhani limeanza kupungua taratibu," alisema kocha huyo raia wa Ujerumani.
Katika msimamo wa Yanga yenye pointi 27 iko kwenye nafasi ya nne nyuma ya vinara Singida Black Stars, Azam FC zenye pointi 30 kila moja na Simba yenye pointi 28.
Hata hivyo, Simba na Yanga zimecheza michezo mitatu pungufu ukilinganisha na vinara.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED