Gamondi afurahishwa ushindani namba Yanga

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 10:19 AM Jul 26 2024
KOCHA wa Yanga, Miguel Gamondi.
Picha: Mtandao
KOCHA wa Yanga, Miguel Gamondi.

KOCHA wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema ushindani wa namba uliopo sasa ndani ya klabu hiyo umeleta matokeo chanya kuelekea msimu mpya wa ligi na mashindano ya kimataifa.

Miguel, amesema usajili waliofanya msimu huu utawapa matokeo mazuri kwa sababu kila mchezaji anauwezo mkubwa na anataka kuonesha kitu kila anapopata nafasi ya kucheza.

"Kumekuwa na ushindani mkubwa kuanzia mazoezini hadi katika mechi za ushindani za kirafiki. Aidha, usajili tulioufanya una manufaa makubwa sana na nina uhakika timu itafanya vizuri sana msimu ujao kwani wachezaji wenye kwa wenyewe wanashindana kuwania namba," alisema Gamondi.

Alisema kuwa maingizo mapya ndani ya kikosi chake yanachochea ushindani kwa asilimia kubwa na ndicho alichokuwa akikitaka kitokee.

"Mathalani, ukiangalia usajili wetu ulikuwa ni wa kimkakati kwelikweli na hatukutaka kuruhusu wachezaji wetu nyota waondoke hiyo tulifanikiwa kuwabakisha. Fauka na hilo, hatukutaka kurizika na kikosi chetu hivyo tukamua tuongeze nguvu kidogo kuleta ushindani, na tumefanya hivyo na matokeo yake tunayaona," alisema.

Alisema malengo yao makubwa ni kuutetea Ubingwa wa Ligi Kuu, Komba la FA na kufika mbali zaidi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Akizungumzia mchezo wao wa juzi dhidi ya TS Galaxy ambao waliibuka na ushindi wabao 1-0, Gamondi, alisema kilikuwa kipimo kizuri kwao.

"Kila mchezaji aliyepata nafasi alionesha kitu, ulikuwa mchezo mzuri na nimefuruhishwa na kile wachezaji wangu walichokifanya hivyo tunaendelea kujenga timu yetu," alisema Gamondi.

Yanga wanatarajia kucheza mchezo mwingine wa michuano ya Kombe la Toyota dhidi ya Kaizer Chief kabla ya kurejea nchini kwa ajili ya tamasha la 'Wiki ya Mwananchi' litakalofanyika Agosti 4.