Dube afungua akaunti ya mabao Yanga

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:34 AM Jul 25 2024
MSHAMBULIAJI mpya wa Yanga, Prince Dube.
Picha: Mtandao
MSHAMBULIAJI mpya wa Yanga, Prince Dube.

MSHAMBULIAJI mpya wa Yanga, Prince Dube, jana alifungua akaunti ya mabao katika timu hiyo alipopachika bao pekee katika mechi ya kuwania Kombe la 'Mpumalanga' dhidi ya TS Galaxy kwenye Uwanja wa Kanyamanzane, Afrika Kusini.

Akiwa ameingia kipindi cha pili, alitumia dakika 10 tu kupachika mpira nyavuni na kuipatia Yanga ushindi wa bao 1-0 ukiwa ushindi wa kwanza wa timu hiyo tangu itue Afrika Kusini kwa ajili ya michezo ya kimataifa ya michuano hiyo maalum ikiwa ni sehemu ya maandalizi yao kuelekea msimu mpya.

Dube, akiwa wingi ya kushoto, aliukimbilia mpira mrefu wa chini chini uliopigwa toka nyuma na kumuhadaa beki wa kulia wa timu hiyo, Nkosikhona Radebe, kabla ya kuujaza mpira wavuni kwa mguu wa kushoto.

Mechi hiyo ilionekana kuchangamka kipindi cha pili hasa baada ya Yanga kuingiza wachezaji wake tegemeo, Stephane Aziz Ki, Maxi Nzengeli, Khalid Aucho na nyota wapya Duke Abuya na Clatous Chama.

Mechi ilianza taratibu na kwa kiasi kikubwa kipindi chote cha kwanza haikuwa ya kuvutia, na huenda ni kwa sababu ya Yanga kutumia wachezaji wengi ambao hawawatumii sana kwenye michezo yake muhimu.

Dakika ya 19, Aboutwalim Mshery alilazimika kufanya kazi ya ziada alipotoka langoni ili kutompa nafasi Siphesihle Maduna kuyaona mapana ya goli, na akafanikiwa kwani shuti la mchezaji huyo liliishia mikononi mwake.

Hata hivyo, Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi kama alivyoahidi kuwachezesha karibuni wachezaji wake wote, alilazimika kumfanyia mabadiliko kipa huyo dakika ya 33 na nafasi yake ikatwaliwa na Khomein Aboubakar ambaye amesajiliwa msimu huu akitokea Singida Black Stars na hata yeye pia dakika ya 61 akatoka na kumpisha Diarra.

Yanga nusura iandike bao dakika ya 25, kama mpira wa kichwa uliopigwa na Clement Mzize usingekwenda nje kidogo ya lango la wapinzani wao.

Mzize alikuwa ameruka juu kuunganisha kwa kichwa, mpira wa krosi iliopigwa na Mudathir Yahaya.

Ilikuwa ni dakika ya 37, wakati Qobolwakhe Sibande alipokosa bao la wazi baada ya kubaki na kipa Khomein, lakini mpira ulitoka nje kidogo ya lango.

Kipindi cha pili Yanga iliingia kwa nguvu ikiwa na mastaa wake wote na kufanikiwa kupata bao hilo lililodumu hadi mwisho wa mchezo.

Hata hivyo TS Galaxy itabidi ijilaumu yenyewe kwani ilikosa mkwaju wa penalti kupitia kwa mchezaji wake, Siphesihle Maduna dakika ya 68 baada ya Duke kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari.