Diarra achagua kubakia Yanga

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 12:18 PM Jun 03 2024
Djigui Diarra
Picha: YANGA
Djigui Diarra

BAADA ya kuwapo kwa tetesi za kutakiwa na timu nyingine, kipa chaguo la kwanza la Timu ya Taifa ya Mali na Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, Djigui Diarra, amesema anapenda kuona anabakia na kuendelea kuchukua makombe zaidi akiwa na klabu hiyo.

Akizungumza na Nipashe kabla ya mechi ya fainali ya mashindano ya Kombe la FA dhidi ya Azam FC iliyochezwa jana usiku, Diarra, alisema atafurahi sana endapo Yanga itabeba tena taji la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao pamoja na mashindano mengine mbalimbali watakayoshiriki.

Diarra alisema analifurahia soka la Tanzania na angependa kubakia kuichezea timu hiyo ambayo iko chini ya Kocha Mkuu, Miguel Gamondi.

"Nataka kuona Yanga inafanya vizuri zaidi katika mashindano mbalimbali, mimi bado ni mchezaji wa Yanga, hivyo ningependa kuona tunaendelea kushinda makombe," alisema golikipa huyo.

Kuhusu kubakia au kuondoka nchini, Diarra, alisema endapo atapata ofa nzuri zaidi ya inayotolewa na Yanga, anaamini suala hilo litajadiliwa na viongozi wa klabu yake. 

"Ikitokea kuna ofa kutoka katika klabu nyingine, viongozi wangu ndio wenye kuzungumza, kwa sasa malengo yangu ni kuifanya Yanga kuwa tishio zaidi Afrika.

Aliongeza Yanga imechangia kwa kiasi kikubwa kupandisha kiwango chake huku ikimsaidia kuitwa katika kikosi cha Mali, ambacho alikiongoza kwenye mechi za Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika zilizofanyika mapema mwaka huu nchini Ivory Coast.

"Malengo yangu mengine ni kuendelea kufanya vizuri zaidi kila ninapopata nafasi, kiwango changu kiendelee kuwa juu, kuwa bora na vile vile kuendelea kuisaidia Yanga kufanya vizuri katika mashindano ya kitaifa na kimataifa," Diarra alisema.

Nyota huyo alisema anafurahia maisha yake ndani na Yanga na aliongeza ushirikiano walionao wachezaji, viongozi na mapenzi wanayopata kutoka kwa mashabiki wao ndio msingi pekee wa mafanikio.

"Tuko pamoja sana, tunashirikiana na kusikilizana, umoja wetu ndio umesaidia sisi kufanya vizuri katika kila mechi," aliongeza mlinda mlango huyo.

Diarra ambaye amesimama mechi nyingi zaidi kuliko golikipa mwingine wa Yanga msimu huu, amezidiwa na mlinda mlango wa Coastal Union, Levy Matampi, ambaye amepata 'Clean sheet' nyingi zaidi na kuifanya timu hiyo ya jijini Tanga kumaliza kwenye nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Hata hivyo mapema msimu uliomalizika, Diarra alishindwa kung'ara katika fainali ya Ngao ya Jamii kwenye hatua ya penalti huku Ally Salim wa Simba akiisaidia timu yake kubeba ngao hiyo kwa kudaka penalti tatu.

Yanga inatarajiwa pia kuiwakilisha Tanzania Bara katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati maarufu Kombe la Kagame ambayo yamerejea na yatafanyika mapema mwezi ujao kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani hapa.