CRDB yadhamini FA Cup kwa bilioni 3.7/-

By Saada Akida , Nipashe
Published at 07:15 PM Apr 02 2024
Rais wa TFF, Wallace Karia (kushoto) pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRBD, Abdulmajid Nsekela baada ya kuingia makubaliano mkataba wa miaka mitatu na nusu wa kuwa Mdhamini Mkuu wa Kombe la Shirikisho la Soka nchini maarufu FA Cup.
MPIGAPICHA WETU
Rais wa TFF, Wallace Karia (kushoto) pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRBD, Abdulmajid Nsekela baada ya kuingia makubaliano mkataba wa miaka mitatu na nusu wa kuwa Mdhamini Mkuu wa Kombe la Shirikisho la Soka nchini maarufu FA Cup.

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limeingia ushirikiano na Benki ya CRBD wa mkataba wa miaka mitatu na nusu wa kuwa Mdhamini Mkuu wa Kombe la Shirikisho la Soka nchini maarufu FA Cup wenye thamani ya Sh. bilioni 3.79 pamoja na VAT.

Utiaji saini huo umefanyika katika makao makuu ya Bank hiyo jana, huku udhamini huo ukianzia hatua hii ya 16-bora ya Kombe la FA baada ya makubaliano hayo kufikiwa kati ya TFF na CRBD Bank .

Akizungumza na Nipashe jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRBD, Abdulmajid Nsekela, alisema hivi karibuni walikuwa na ushirikiano na klabu za soka hapa nchini na sasa wameona wauendeleze zaidi kwa kushirikiana na TFF katika kuendeleza soka la Tanzania.

Alisema wameingia makubaliano hayo kwa hatua ya 16-bora ambapo kwa kuanzia hapo wametoa kiasi cha Sh. milioni 255 kwa ajili ya kumalia hatua hiyo na baadae wataendelea kwa misimu mingine.

“Udhamini huu unaenda kuboresha mambo mbalimbali ila kwa sasa tumeamua kutoa kiasi cha Sh. milioni 255 kumalizia hatua hii ya 16-bora ambayo inaanza kuchezwa leo (jana) kati ya Namungo FC na Kagera Sugar.

"Tumeona jinsi ambavyo TFF inavyosimamia soka na kufanya vizuri kwa timu za taifa ikiwamo Taifa Stars, Twiga Stars na timu za vijana kuipeperusha vema bendera yetu ya Tanzania,” alisema Msekela.

Kwa upande wa rais wa TFF, Wallace Karia, alisema ni tukio la kihistoria kwa kusaini mkataba wa udhamini mkuu wa kwanza katika mashindano haya ya Kombe la Shirikisho ambayo awali ilijulika kama Azam Sport Federation na sasa inaenda kuwa CRDB Bank Federation.

Alisema mchakato umehitimishwa jana baada ya mazungumzo ya muda mrefu na CRDB kuwa wadhamini wa kwanza wa mashindano hayo ambaYo awali yalikuwa chini ya Azam kwa sababu ya kuwa na haki za kuonyesha michezo hiyo.

“Kwa mara ya kwanza Kombe la Shirikisho linapata mdhamini mkuu ambaye ni CRBD Bank kwa mkataba wenye thamani ya Sh. bilioni 3.2 baada ya VAT,  mashindano haya yanashirikisha timu nyingi  zaidi ya 100, yanaamzia chini tangu level ya wilaya.

"Ninaimani mashindano ya CRBD Bank Federation yanaenda vizuri na fedha zitaenda katika sehemu husika kwa timu kusaidia mambo mbalimbali ikiwamo usafiri na mahitaji muhimu,” alisema Karia.

Aliongeza kuwa wao kama shirikisho walikutana na kuona fainali za FA, msimu huu zitafanyika katika Uwanja wa Tanzanite uliopo Babati mkoani Manyara, baada ya kujiridhisha na ubora wa miundombinu yao ikiwamo uwanja.

Aidha, alisema msimu huu nusu fainali zitakuwa mbili, moja itafanyika jijini Mwanza na ya pili bado haijulikana mkoa gani itacheza kwa sababu ya mikoa kuendelea kufanya ukarabati wa viwanja vyao.

“Nafasi ipo wazi kwa mkoa ambao utakidhi miundombinu yao ikiwamo uwanja, tunapeleka mikoani kwa ajili ya kutoa shukurani hasa katika mikoa hiyo inayofanya ukarabati wa viwanja vyao,” alisema Karia.