Biashara United mguu mmoja Ligi Kuu

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:12 AM May 21 2024
Klabu ya Biashara United.
Picha: Mtandaoni
Klabu ya Biashara United.

KLABU ya Biashara United tayari imetanguliza mguu mmoja kurejea kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya juzi kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Karume, Musoma dhidi ya Mbeya Kwanza kwenye mchezo wa kwanza wa 'Play off'.

Biashara iliyoshuka daraja msimu wa 2021/22 sasa itasubiri mechi ya marudiano itakayochezwa Jumapili ijayo, Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara, kujua kama watarejea Ligi Kuu. 

Timu inatakiwa kulinda ushindi wake huo kwa kulazimisha sare yoyote, au kupoteza mechi kwa idadi isiyozidi bao 1-0 ili kusonga mbele.

Kwa upande wa Mbeya Kwanza ambayo nayo ilishuka kutoka Ligi Kuu msimu wa 2021/22, italazimika kupata ushindi wa mabao 3-0 nyumbani ili kupita hatua hiyo.

Mabao ya Biashara juzi yalifungwa na Abeid Athumani na Boban Zirintusa.

Biashara United na Mbeya Kwanza zililazimika kucheza michezo ya ‘Play Off’, baada ya kumaliza nafasi ya tatu na ya nne katika Ligi ya ‘Championship’.

Mbeya Kwanza ilimaliza nafasi ya tatu na pointi zake 65, Biashara United ikiwa ya nne ilikusanya pointi 62, huku ikiziacha timu za Ken Gold na Pamba zikipanda Ligi Kuu moja kwa moja.