Balozi: Kwa Simba hii timu zijipange

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:13 AM Jul 24 2024
Balozi wa Tanzania nchini Misri, Meja Jenerali Richard Mutayoba Makanzo.
Picha: Simba SC
Balozi wa Tanzania nchini Misri, Meja Jenerali Richard Mutayoba Makanzo.

WAKATI Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, akionekana kufurahishwa na ushindi ambao timu yake iliupata juzi dhidi ya El Qanah, lakini akisema bado anahitaji muda ili wachezaji wake wafanye vile anavyotaka, Balozi wa Tanzania nchini Misri, Meja Jenerali Richard Mutayoba Makanzo, amekimwagia sifa kikosi hicho, akizitahadharisha timu za Ligi Kuu Tanzania Bara zijipange kukabiliana nayo.

Akizungumza baada ya mechi ya kirafiki na timu hiyo inayocheza Ligi Daraja la Pili, iliyochezwa Ismailia nchini Misri, Simba ikishinda mabao 3-0, Balozi huyo aliwasifia watu waliofanya usajili wa wachezaji hao, akisema kwa macho yake amekuwa mmoja kati ya Watanzania wa mwanzo kukiona kikosi hicho, chenye wachezaji wanaotandaza kandanda la uhakika.

"Naipongeza timu iliyofanya usajili kwa kweli imesajili vijana wazuri sana, nimewaona mwenyewe kwa macho yangu, wanacheza mpira safi sana, na tuseme tu msimu unaoanza timu nyingine nyumbani zijipange, Simba wako vizuri sana," alisema Makanzo.

Balozi huyo ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mchezo huo uliopigwa juzi jioni katika Uwanja wa Old Suez Canal, alisema atakuwa na kikosi hicho kipindi chote ambacho watakuwa nchini humo, ikiwamo kurejea tena kuwapa nguvu katika mchezo mwingine utakaofuata.

"Mimi kama balozi, nawaahidi nitakuwa nanyi kwa kipindi chote mtakachokuwa hapa Misri na nitakuja tena ili kuwapa nguvu kwa mchezo utakaofuata, hongereni kwa ushindi mzuri, lakini kikubwa tulikuwa tunatazama jinsi mnavyocheza.

"Mngeamua kukaa Tanzania, lakini mmeamua kuja kukaa huku, tunajua ni gharama, lakini mmefanya heshima kwa nchi yetu kwa sababu mnaimarisha diplomasia ya mpira wa miguu na michezo kwa ujumla, hiki mlichokifanya mnatuongezea tuwe na mahusiano mazuri na nchi hii, hongereni sana," alisema.

Katika mechi hiyo, Simba ilishinda mabao 3-0, katika mchezo uliochezwa kwa dakika 120, kwa vipindi vitatu vilivyochezwa kwa dakika 40 kila kipindi.

Mabao ya Simba yalifungwa na wachezaji wapya ambao ni Jean Charles Ahoua, aliyesajiliwa kutoka Stella Club d'Adjame ya nchini Ivory Coast, dakika ya 14 na 16, na Augustine Okejepha namba sita ya 'boli' kutoka Rivers United ya Nigeria dakika ya 120.

Kocha Fadlu baada ya mechi hiyo alisema anajivunia ushindi wa vijana wake, lakini akisema anahitaji muda zaidi ili wawe fiti kwani wana wiki mbili tu, ambapo ili waweze kucheza anavyohitaji anahitaji wiki nne mpaka tano.

"Inapaswa tujivunie na ushindi huu, mimi mwenyewe nina furaha, tulikuwa na wiki mbili ngumu ya kukiandaa kikosi, tulikuwa tunahitaji kucheza na kushinda, lakini tulihitaji pia wachezaji wetu wawe na muunganiko na mawasiliano baina yao wenyewe uwanjani.

Baadhi ya wachezaji wamecheza dakika 60, wakati mwingine nilifanya mabadiliko kutokana na jinsi ninavyoona mchezo unavyokwenda, tulianza vizuri tukafunga mabao mawili haraka, tukapoteza nafasi nyingi hasa kipindi cha kwanza, bado hatuna uwezo wa kucheza dakika zote 90 kwa kasi ile ile, kwa sababu tuna wiki mbili tu, tunahitaji kiasi cha wiki nne au tano za mazoezi, tunahitaji muda," alisema.