Aziz Ki ambwaga Chama, Fei Toto

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 06:49 PM Apr 02 2024
Kiungo Mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz Ki.
MAKTABA
Kiungo Mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz Ki.

KIUNGO Mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz Ki, amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara mwezi Machi, huku Kocha Mkuu wa Azam FC, Bruno Ferry naye akitwaa tuzo ya kocha bora wa ligi hiyo kwa mwezi huo.

Taarifa ilioyotolewa jana mchana na Idara ya Habari na Mawasiliano ya Bodi ya Ligi Kuu, imesema kuwa washindi hao wamechaguliwa na Kamati ya Tuzo ambayo pia imemchagua Meneja wa Uwanja wa Lake Tanganyika uliopo Kigoma, Shaaban Rajab, kuwa meneja bora wa mwezi uliopita.

Aziz Ki, mchezaji wa Timu ya Taifa ya Burkina Faso, amewashinda viungo washambuliaji wenzake ambao ni Clatous Chama wa Simba, ambaye anaichezea Timu ya Taifa ya Zambia na Feisal Salum wa Azam, ambaye pia ni mchezaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars.

Kamati imesema kwa Machi, Aziz Ki alionyesha kiwango kikubwa na kuisaidia timu yake kupata ushindi katika michezo mitatu kati ya minne ambayo timu yake imecheza, akifunga mabao matatu na kuhusika na mengine manne.

Aliifunga Ihefu mabao 5-0, Geita Gold bao 1-0, Namungo mabao 3-1, lakini ikapoteza kwa Azam 2-1, Aziz Ki akicheza jumla ya dakika 330 katika michezo hiyo.

Kwa mujibu wa takwimu za Dawati la Nipashe, Aziz Ki, mbali na kuwa kinara wa kufunga mabao kwenye Ligi Kuu akiwa nayo 13 akiwa sawa na Fei Toto, ametoa pasi za usaidizi saba mpaka sasa, hivyo pia anaongoza kwa kuisaidia timu yake ya Yanga jumla ya mabao 20 hadi kufikia sasa.

Kwa upande wa Bruno, amewashinda Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi na Zuberi Katwila wa Mtibwa Sugar ambao aliingia nao fainali.