Azam yaanza kujipanga kimataifa

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:38 AM May 27 2024
 Azam FC imeendela kuimarisha kikosi chake kuelekea msimu ujao baada ya kumtambulisha kiungo mpya, Ever Meza iliyemnunua kutoka klabu ya Leonnes ya kwao, Colombia.
Picha: Mtanfaoni
Azam FC imeendela kuimarisha kikosi chake kuelekea msimu ujao baada ya kumtambulisha kiungo mpya, Ever Meza iliyemnunua kutoka klabu ya Leonnes ya kwao, Colombia.

WAKATI ikikaribia kukata tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao, klabu ya Azam FC imeendelea kufanya usajili wake mapema kabisa baada ya kukamilisha uhamisho wa mchezaji Ever Meza kutoka klabu ya Leonnes FC ya Colombia.

Taarifa iliyotolewa jana na klabu hiyo, imesema mchezaji hiyo anayecheza nafasi ya kiungo mkabaji, aliyezaliwa Julai 21, 2000, amesaini mkataba wa miaka minne, utakaombakisha hadi 2028 kwenye viunga vya Chamazi, Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya kutia saini mkataba huo, mchezaji huyo aliwataka mashabiki wa timu hiyo kutegemea mazuri kutoka kwake kwani yeye ni mchezaji jasiri.

"Kwanza najisikia furaha kuwa mahali kama hapa, nawaahidi mashabiki wa Azam FC wategemee kitu kizuri kutoka kwangu, mimi ni mchezaji jasiri, mpambanaji na mshindani sana," alisema Meza, ambaye alikuwa anaichezea klabu ya Alianza FC ya Colombia kwa mkopo, huku klabu mama ikiwa ni Leonnes FC .

Habari kutoka ndani ya Azam FC zinasema, klabu hiyo imetumia kiasi cha takribani Sh. milioni 845 kwa ajili ya kuinasa saini ya kiungo huyo.

Meza, anakuwa mchezaji wa pili kusajiliwa kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kwani tayari klabu hiyo imemshusha beki wa kati Yoro Mamadou Diaby aliyekuwa akiichezea klabu ya Stade Malien de Bamako ya nchini Mali.

Chanzo kingine kutoka Azam, kinasema klabu hiyo huenda ikamsajili mshambuliaji wa Mashujaa FC, Adam Adam, ambaye tayari ameshaagana na timu hiyo.

Azam ina tiketi ya kucheza michuano ya kimataifa msimu ujao, ingawa mpaka sasa haijajulikana kama ni Ligi ya Mabingwa Afrika au Kombe la Shirikisho mpaka baada ya matokeo ya mechi yake ya mwisho kesho dhidi ya Geita Gold, Uwanja wa Nyankumbu, Geita.