Maofisa Malawi waongezewa uelewa mtaala ulioboresha nchini

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 07:14 PM Aug 13 2024
Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Tanzania Dk. Aneth Komba kulia akieleza jambo kwa wajumbe wa Elimu kutoka Malazi.
Picha: Mpigapicha Wetu.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Tanzania Dk. Aneth Komba kulia akieleza jambo kwa wajumbe wa Elimu kutoka Malazi.

MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dk. Aneth Komba ameongoza kikao cha wajumbe wa menejimeti na ujumbe wa Taasisi ya elimu ya Malawi kikiwa na lengo la kutoa fursa kwa wawakilishi hao wa Malawi kujifunza kuhusu mabaoresho ya mtaala yaliyofanyika nchini 2023.

Katika kikao hicho ambacho kimefanyika leo mkoani Dar es Salaam ujumbe wa Malawi umeongozwa na Mratibu wa Mitaala ya elimu ya msingi katika Taasisi ya Elimu ya Malawi, Michael Simawo ambaye amesema kuwa lengo la ziara yao ni kutaka kufahamu namna Tanzania imefanya katika maboresho ya Mtaala wa elimu.

“Tumefurahia kufika Tanzania na kufahamu masuala mbalimbali yahusuyo mfumo wa elimu nchini ambako tulianzia Wizara ya elimu, Sayansi na Teknolojia na sasa tumemaliza hapa TET  ili tujifunze zaidi kwani tuko kwenye harakati za kuboresha elimu yetu,” amesema Simawo.

Ameongeza kuwa, wako katika hatua za mwisho za maboresho ya mitaala ya elimu, ndio maana waliona umuhimu wa kupita katika nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania ili wajifunze njia zilizotumika kufanikisha maboresho ya mitaala hiyo.

1

Dk. Komba amesema kuwa ni jambo jema kwa nchi ya Malawi kujifunza juu ya Mitaala ya Tanzania, na kwamba ni vizuri kupata uzoefu wa nchini nyingine ambao utasaidia katika kuboresha elimu yao.

Katika kikao hicho, Dk. Komba amewaeleza hatua mbalimbali zilizopitiwa katika maboresho ya mitaala ya elimu na namna yalivyoanza kufanyika katika baadhi ya ngazi ya madarasa nchini.

Pia ujumbe huo umepata nafasi ya kujionea darasa janja (Smart class) namna linavyofanya kazi kwa wakati mmoja inapoweza kutumika kufundishia na kijifunzia kwa walimu zaidi ya 300 na kuangalia studio za kurekodi sauti na video mbalimbali za kielimu.

2