Dk. Biteko atoa maagizo kwa mawaziri, makatibu wakuu kutumia mfumo NeST

By Allan Isack , Nipashe
Published at 03:14 PM Sep 10 2024
Naibu Waziri Mkuu,Dk.Dotto Biteko
Picha: Mpigapicha Wetu
Naibu Waziri Mkuu,Dk.Dotto Biteko

RAIS Dk.Samia Suluhu Hassan,amewaagiza Mawaziri na Makatibu Wakuu, kuhakikisha kuwa taasisi zote za Umma zinatumia mfumo wa wa kielekroniki wa NeST katika manunuzi yote ya serikali ili kuongeza ufanisi.

Hayo yalisemwa jana jijini Arusha na Naibu Waziri Mkuu,Dk.Dotto Biteko,akifungua kongamano la 16 la ununuzi wa Umma kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa niaba ya Rais Dk.Samia, lenye kaulimbiu ya ‘Matumizi ya TEHAMA kwenye manunuzi ya Umma Endelevu’.

“Ninawaelekeza pia Mawaziri na Makatibu Wakuu wote kuhakikisha kuwa taasisi nunuzi zilizopo kwenye mafungu yenu, pamoja na taasisi zote za umma,zinautumia mfumo wa NeST katika ununuzi wote unaotumia fedha za serikali,”alisema Dk.Biteko. 

Alisema pamoja na jitihada za Serikali kujenga NeST, inashangaza kuona kuwa kuna baadhi ya taasisi za umma hazitumii mfumo huo katika shughuli za ununuzi.

“Ninatoa maelekezo kwa Waziri kwa kushirikiana na Mamlaka nyingine kama vile Msajili wa Hazina,kuhakikisha kwamba wote ambao wamepewa majukumu ya kuongoza taasisi za umma wahakikishe wanatumia NeST,”alisema.

Dk.Biteko ambaye pia ni Waziri wa Nishati,alisema mfumo huo kwa Tanzania umeleta manufaa makubwa kwa kuwa umepunguza kwa gharama za kufanya ununuzi kwa wazabuni na Serikali, kuondokana na matumizi ya karatasi,kuongezeka kwa kasi ya ununuzi,kupungua kwa makosa katika ununuzi na kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.

“Nimefurahi kusikia  mfumo huu niliouzindua pia umeongeza uwazi, uwajibikaji na kuleta thamani ya fedha katika ununuzi ni wazi kuwa mfumo huu utaleta faida nyingine nyingi ikiwemo kuimarisha utawala bora,kuongeza wigo wa ununuzi na kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa,”aliongeza. 

Aidha alisema Serikali imeendelea kudhibiti matumizi ya fedha zinazopelekwa kwenye kila fungu kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo mifumo ya kielektroniki ili kuleta tija na ufanisi unaostahili katika utekelezaji wa Bajeti ya fungu husika. 

Alisema ya Tanzania imefanya mageuzi makubwa ya kisheria katika ununuzi wa umma ambayo yalianza Mwaka 2001 kwa kutungwa kwa sheria ya kwanza ya Ununuzi wa Umma, baada ya changamoto kadhaa, zilizosababisha mabadiliko ya Sheria ya mwaka 2004, na kuanzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).

Kadhalika ametoa rai kwa Sekretarieti ya EAC kuhakikisha masuala ya pamoja ya ununuzi wa Umma yanajadiliwa kwenye vikao vya ngazi mbalimbali za Jumuiya hiyo kwa ustawi wan chi wanachama.

”Katika Jumuiya  ya Afrika Mashariki,  tunajua vyema haja ya kuwa na mifumo imara ya kidigitali katika nchi zetu, kwa lengo la kuendeza ustawi wa uchumi kwenye nchi zetu kwa kuwa dunia hii ya kidigitali na kadiri ushirikiano unavyokuwa, nchi zetu zitaendelea kufaidika zaidi ikiwa tutaendeleza matumizi ya digitali kwenye shughuli zetu za kiuchumi,”alisema.

Mkurugenzi Mkuu wa PPRA,Denis Simba,alisema katika jukwaa hilo mada mbalimbali zitawasilishwa ikiwamo mafanikio na changamoto za mfumo wa ununuzi,teknolojia inavyoweza kuleta mabadiliko katika sekta hiyo na namna nchi wanachama watavyoweza kuboresha ununuzi katika ukanda wa EAC.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya PPRA,Leonada Magire,alisema hadi kufikia Agosti 31 2024, jumla ya taasisi nunuzi 1151 zimeweza kuuhisha taarifa na kuanza kutumia mfumo huo.

Pia alisema jumla ya taasisi nunuzi 148 zilitangaza mipango ya ununuzi wa mwaka zenye thamani ya trilioni 31.9 ambapo wazabuni 21,991 walisajaliwa na kuidhinishwa ndani ya mfumo kati ya wazabuni hao 21094 ni wa ndani 897 ni wa nje nchi.

“Jumla ya zabuni 39837 zilitangazwa na tuzo za zabuni 34908 zenye thamani ya shilingi trilioni 5.6 zimetolewa”.