Wapendekeza wanaojaribu kujiua kuondolewa adhabu

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 10:50 AM Sep 10 2024
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Michelle Chapa Foundation, Dk. Michelle Chapa
Picha: Nipashe Digital
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Michelle Chapa Foundation, Dk. Michelle Chapa

WATETEZI haki na afya ya binadamu wamependekeza kuondolewa kwa sheria ya adhabu kwa watu wanaojaribu kujiua.

Badala yake wamependekeza kuwapo kwa wigo wa uponyaji kisaikolojia na usaidizi wa afya ya akili.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Michelle Chapa Foundation, Dk. Michelle Chapa, alisema hayo wakati wa kampeni ya kuondoa Sheria ya Adhabu ya Kujiua nchini, katika mada iliyoendeshwa mtandaoni, iliyoandaliwa na Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe.

Dk. Michelle alisema kuondolewa kwa sheria hiyo kutabadilisha mazungumzo kuhusu kitendo hicho, kwa kuondoa lawama kwa wanaotenda matukio hayo kwa kuwa wengi wao sababu kuu ni kuzongwa na magonjwa ya akili.

Kwa mujibu wa kifungu cha 217 cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16, kujaribu kujiua ni kosa la jinai; linaweza kuhukumiwa kwa adhabu isiyozidi miaka mitano jela, kama inavyoelekezwa na kifungu cha 35 kinachoeleza adhabu ya jumla kwa makosa ambayo hayajapewa adhabu ya moja kwa moja. 

Pia, sheria hiyo inaweka kinga katika kifungu cha 13 na inatoa msamaha kwa watu wanaofanya makosa wakiwa katika hali ya ugonjwa unaoathiri akili zao na kufanya wasielewe wanachofanya.

Dk. Michelle, alisema lengo la mada hiyo ni kukuza uelewa kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kujizuia Kujiua Duniani, inayofanyika Septemba 10, kila mwaka.

Alisema matukio ya aina hiyo huwa hayazungumziwi sana katika jamii na kuna sababu nyingi, ikiwamo mila, unyanyapaa na kwamba wadau mbalimbali kama vile Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe (MNMH), wamemekuwa wakiiadhimisha siku hiyo, kwa kuwapo makongamano.

Mwanasheria Jebra Kambole, alisema kesi za aina hiyo zipo na tayari huwa zimefikishwa katika mahakama na kwamba adhabu hiyo imeendelea kutekelezwa nchini kutokana na kurithiwa kutoka kwa wakoloni, ambao kwa sasa hata wao hawaitumii tena.

Alisema ni vyema jamii ikaelewa kwamba kukaribia kufanya kosa hilo ni jinai, hivyo mapendekezo ni kwamba mtu aliyejaribu huhitaji tiba kiafya na ndiyo sababu ya wadau kuhamasisha kuondolewa kwa adhabu hiyo. 

Alisema: “Ni kosa la kikoloni na wao walishaliondoa kwao, sisi bado tumeikumbatia, watu wanaojaribu kufanya kosa hilo wanahitaji tiba ya kisaikolojia, kwa sababu hata akifungwa ile nia yake atakuwa nayo. Zamani pia katika familia ikitokea mtu kafanya kosa hilo, aliadhibiwa kwa kutengwa.”