JESHI la Polisi mkoani Tanga linamsaka Dismas Yohana, mkazi wa Kijiji cha Kwafungo, wilayani Muheza kwa tuhuma za kusababisha kifo cha mtoto wake, Aloni Dismas mwenye umri wa miezi saba.
Kamanda wa Polisi mkoani Tanga, Almachius Mchunguzi alisema jana kuwa Yohana anadaiwa kusababisha kifo cha mtoto wake wakati anagombana na mkewe, Sharifa Omari, ndipo alimwangukia mtoto huyo aliyekuwa amelala kitandani.
Kamanda Muchunguzi alisema tukio hilo lilitokea juzi usiku katika kijiji hicho ambako mtuhumiwa huyo alikuwa anaishi na familia yake.
Alisema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo kubaini chanzo cha ugomvi.
Mmoja wa ndugu wa familia, Matha Joseph alisema kuwa ulitokea ugomvi usiku kati ya wanandoa hao uliosababisha kupigana na kumwangukia mtoto wao huyo ambaye alikimbizwa Hospitali Teule ya Muheza, lakini alifariki dunia.
Alisema kuwa baada ya ugomvi wa wanandoa hao, mke aliondoka nyumbani usiku majira ya saa mbili mpaka Kituo cha Polisi Muheza Mjini kutoa taarifa, kisha kwenda Hospitali Teule ya Muheza kwa ajili ya matibabu ya mtoto.
Alisema kuwa ilipofika saa tano usiku, mtoto huyo alifariki dunia na mama yake alitibiwa na kupewa rukhsa kwenda nyumbani.
Alisema kuwa mtoto huyo ameshazikwa katika Kijiji cha Maskati, Kata ya Bwembwera, wilayani Muheza na kwamba mtuhumiwa ametoroka, anatafutwa na Jeshi la Polisi.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED