MAKAMU wa Rais, Dk. Philip Mpango, amesema hali ya mazingira nchini ni mbaya na wastani wa hekta 24,151 za misitu zinazopotea kila mwaka huku akitaja sababu kadhaa ikiwamo inayotuhumu baadhi ya wafanyabiashara wa mkaa kuwa ni watoa maamuzi na wana maslahi binafsi.
Akizungumza jana kwenye mkutano maalum wa viongozi, wataalamu na wadau wa mazingira kuhusu hali ya mazingira nchini, Dk. Mpango alisema: “Tanzania inalia, athari za uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi ni kubwa sana zimetuathiri kwa kiasi kikubwa sana, zinahatarisha uhai wa viumbe vyote ikiwamo sisi wanadamu, usalama wa chakula, upatikanaji wa maji na magonjwa ya mlipuko.”
Alisema taarifa ya nne ya mazingira ya mwaka 2024 inaonesha hali ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira nchini haliridhishi.
“Nchi yetu inakabiliwa na changamoto mbalimbali za mazingira ambazo kwa kiasi kikubwa zinatokana na tabia ya watu, ukataji ovyo wa miti na uharibifu wa misitu ambapo takwimu zinaonesha ongezeko kubwa la uharibifu wa misitu kutoka hekta 372,816 kwa mwaka 2019 hadi 469,420 kwa mwaka 2023,” alisema.
Alisema wastani wa hekta 24,151 zinazopotea kila mwaka na uharibifu huo unachangiwa kwa sehemu kubwa na shughuli za binadamu zisizo endelevu ikiwamo utegemezi mkubwa wa nishati ya kuni na mkaa.
Kadhalika, alisema takwimu zinaonesha kuwa tani milioni saba za taka ngumu zinazalishwa nchini kila mwaka ambapo wastani wa tani milioni 3.5 ndio zinazokusanywa na kutupwa maeneo yanayostahili na zilizobaki hutupwa ovyo.
“Katika matumizi ya nishati chafu, takwimu za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, asilimia 82 za nishati inayotumika kwa ajili ya kupikia inatokana na kuni na mkaa, matumizi ya nishati chafu inasababisha ukataji wa miti ili kukidhi mahitaji makubwa ya nishati ya kupikia,” alisema.
Alisema moja ya sababu zinazochangia hali ya mazingira kutokuwa nzuri ni pamoja na uwapo wa sheria kinzani na kutolea mfano sheria iliyounda Wakala wa Misitu (TFS) bado inafanya mkaa kuwa chanzo cha mapato na inahamasisha utoaji wa vibali vya kukata miti ili kutengeneza mkaa.
Alisema anachoona ni kasi ya ukataji miti isiyoendana na kasi ya upandaji miti, bado elimu kwa umma haitoshi ikiwamo kubadili mazoea kwenye kilimo.
“Badala ya kulima kwa kuchoma moto kuandaa mashamba, lakini bado wananchi wetu hawatusikii, kwa hiyo pengine nafikiri namna yetu ya kutoa elimu kwa umma haiendi kwa namna ambayo watu wetu wanaelewa, tunahitaji kujitazama vizuri, tutumie mbinu gani ili elimu hii iwafikie wananchi wetu,” alisema.
“Wenye kipato kidogo wanashindwa kumudu teknolojia za kijani za nishati safi ya kupikia na serikali ina uwezo mdogo wa kutoa ruzuku, hizi changamoto naamini kupitia mkutano huu itazijadili na kuja na mapendekezo ya namna ya kwenda mbele ili Tanzania iache kulia kutokana na uharibifu wa mazingira.”
Alitaka mkutano huo uainishe namna bora ya kufikia matokeo tarajiwa kwa kutafuta majibu ya changamoto za kimazingira zilizopo ikiwamo usimamizi wa mazingira nchini.
Alimwagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Muungano na Mazingira, Dk. Ashatu Kijaji, kuwasilisha kwake taarifa ya mkutano huo na mapendekezo yatakayotolewa mapema iwezekanavyo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dk. Ashatu Kijaji, alisema kupitia mkutano huo mada nane zitajadiliwa ikiwamo ya biashara ya kaboni na inatarajiwa kuongeza hamasa ya uwajibikaji katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira nchini.
Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Harusi Said Suleiman, alisema Zanzibar imeathiriwa na mabadiliko ya tabianchi kwenye mazingira na Agosti 17, mwaka huu walizindua programu ya kuirudisha Zanzibar ya kijani.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED