WALIMU wa shule za msingi na sekondari wilayani Tarime mkoani Mara pamoja na watendaji wa kata zinazotekelezwa mradi wa jamii imara wamepewa mbinu mbadala za nidhamu na kudhibiti ukeketaji kwa watoto wa kike.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo yaliyotolewa na shirika lisilo la serikali la Wildaf wilayani Tarime, Ofisa Mradi wa Jamii Imara, Suzan Kawanga alisema mbinu zinazotolewa zinalenga kumsaidia mwalimu kusimamia vema darasa na kuwalinda watoto dhidi ya ukatili.
Kadhalika alisema wanamjengea mwalimu mazingira ya kujifunza mbinu salama na mbadala ya adhabu za kimwili kama vile kazi za kijamii, majadiliano ya pamoja, shughuli za kujenga uhusiano mzuri kati yao na wanafunzi.
Mtoa mada katika mafunzo hayo, Thomas Mponda alisema kwa walimu walezi wanatakiwa kutambua mbinu bora za malezi kwa wanafunzi na jinsi ya kujihami na ukatili wa kijinsia hususani ukeketaji. Mponda alisema lengo la kuwaweka pamoja walimu, viongozi wa serikali pamoja na kinamama ni kuhakikisha watoto wanakuwa salama dhidi ya ukatili wa ukeketaji kwani hayo ndiyo maeneo yanayomzunguka kila siku.
Mtendaji Kata ya Komaswa, Joyce Mwita aliomba Bunge kutunga sheria kali dhidi ya ukatili kwa watoto na wanawake ili kuwaadhibu wote wanaojihusisha na vitendo hivyo na kuomba elimu iendelee kutolewa kwa jamii.
Baadhi ya washiriki katika mafunzo hayo, Anna Nyamohanga alisema kuwa wazazi wanapaswa kuwasomesha watoto wa kike ili waondokane na tabia ya kuwakeketa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED