Waziri ataka wazazi kuandaa jina la mtoto kabla hajazaliwa

By Kulwa Mzee , Nipashe
Published at 09:30 AM Aug 13 2024
Waziri wa Katiba na Sheria Balozi Dk. Pindi Chana Agosti 09, 2024 alifanya ziara na kukagua zoezi la usajili na kuwapatia vyeti vya kuzaliwa watoto wa umri chini ya miaka mitano katika hospitali ya  St.Gemma, kituo cha afya Makole.
Picha: Mtandao
Waziri wa Katiba na Sheria Balozi Dk. Pindi Chana Agosti 09, 2024 alifanya ziara na kukagua zoezi la usajili na kuwapatia vyeti vya kuzaliwa watoto wa umri chini ya miaka mitano katika hospitali ya St.Gemma, kituo cha afya Makole.

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Balozi Dk. Pindi Chana, ameomba wazazi kuandaa majina ya watoto wao kabla ya kuzaliwa ili kwa haraka wasajiliwe na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa baada ya kuzaliwa.

Balozi Dk. Chana alitoa rai hiyo mwishoni mwa wiki jijini Dodoma wakati wa ziara yake ya kujionea usajili unavyoendelea na kuwapatia vyeti vya kuzaliwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano katika Hospitali ya St. Gemma, Kituo cha Afya Makole na Zahanati ya Kikuyu, jijini humo.

"Leo nimetoa vyeti vya kuzaliwa kwa baadhi ya kinamama waliojifungua salama na kuruhusiwa kwenda nyumbani. Ninaomba wazazi kujenga utaratibu wa kuandaa jina la mtoto mapema kabla ya kuzaliwa ili asajiliwe baada ya kuzaliwa na kupatiwa cheti kwani ni haki ya kila Mtanzania," alisisitiza.

Waziri Chana alielekeza taasisi za umma na binafsi kupokea vyeti hivyo vinavyojazwa kwa mkono na kutolewa kwa wototo wa umri chini ya miaka mitano wanaosajiliwa katika ofisi za watendaji kata na vituo vya tiba kote nchini kwa kuwa ni vyeti halali na vina hadhi sawa na vyeti vinavyotolewa kwa njia ya kompyuta.

Balozi Dk. Chana pia aliwataka wananchi kuchangamkia huduma hiyo inayotolewa bure nchi nzima, akisema kuwa vyeti hivyo vina mchango mkubwa katika kupata huduma mbalimbali, ikiwamo matibabu kupitia bima ya afya, elimu na baadaye ajira na kuzitaka taasisi mbalimbali za umma na binafsi kupokea vyeti hivyo kwa ajili ya kuwapata wananchi huduma.

“Nipende kupongeza Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa kazi kubwa wanayoifanya ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Watanzania wanapata vyeti vyao vya kuzaliwa na hili nimejiridhisha pasi na shaka kazi hii kubwa ikiendelea kwa ufanisi mkubwa," alisema.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Makole, Dk. Flora Mwakalago alisema kuwa tangu kuanzishwa huduma za usajili wa vizazi kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano mwaka 2019, zaidi ya watoto wachanga 550-600 huzaliwa kila mwezi huku kati yao, watoto 200- 250 wakipatiwa vyeti vya kuzaliwa.

"Kwa kipindi cha mwezi Julai 2023 hadi Juni 2024, tayari tumeshasajili na kuwapa vyeti vya kuzaliwa watoto zaidi ya 2,750. Haya ni matokeo mazuri kwa kituo chetu," alisema Dk. Mwakalago.

Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Kikuyu, Dk. Azania Silliah alisema kata ya Kikuyu Kaskazini ina jumla ya wakazi 14,654 (wanawake 9,250).

"Kuanzia mwezi Julai mwaka jana (2023) mpaka kufikia mwezi Juni 2024, tumesajili na kuwapatia vyeti watoto zaidi ya 642 sawa na asilimia 92," alisema Dk. Silliah.

Mmoja wa wazazi waliopatiwa vyeti, Halima Abdallah, mbali ya kushukuru serikali kwa kuboresha na kujenga vituo vya afya, alisema kuwapo huduma hiyo inayotolewa bure nchi nzima kumekuwa mkombozi kwa kuwa kila mtoto anapata cheti cha kuzaliwa mara tu baada ya  kuzaliwa na hivyo kuokoa gharama  ambazo zingezitumika kukipata kwenye ofisi za RITA.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Frank Kanyusi, alisema tangu zoezi hilo la kusajili watoto wote chini ya miaka mitano, watoto wengi wamesajiliwa nchini nzima na mwamko umekuwa mkubwa.