Dk. Tindwa apongeza lugha ya kichina kufundishwa Shule ya Ujenzi

By Yasmine Protace , Nipashe
Published at 07:47 PM Aug 12 2024
Wanafunzi Shule ya Ujenzi.
Picha: Mpigapicha Wetu
Wanafunzi Shule ya Ujenzi.

MJUMBE wa Kamati ya Uchumi ya Jumuiya ya Wazazi Taifa (CCM) Dk. Chakou Halfan Tindwa , ameipongeza Taasisi ya MHL kwa kufundisha lugha ya kichina katika shule zake.

Dk. Tindwa ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tindwa Medical and Health Services ametoa kauli hiyo wakati wa mahafali  ya Shule ya awali na msingi katika Shule ya Ujenzi iliyopo Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.

Alisema kuwa Taasisi ya MHL kufundisha lugha ya kichina katika shule zake itawasaidia wahitimu kunufaika na lugha hiyo kutokana raia wengi kutoka China kuja kuwekeza Tanzania.

"Naipongeza Taasisi ya MHL kwa kufundisha lugha ya kichina kwa wanafunzi wake,kwa kuwa sasa tunawawekezaji wengi wa kichina na kuna viwanda vingi nchini.Pia naipongeza taasisi hii kwa kuwafundisha wanafunzi wa elimu ya msingi hadi sekondari masomo ya ujasiliamali kwani kwa kufanya hivyo kunawasaidia wanafunzi kujipatia kipato na kuacha kuwa tegemezi" alisema

Dk. Tindwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Tanzania Health Summit alikuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo. "Ni jambo jema ambalo uongozi wa MHL mmelifanya kwa kuwafundisha wanafunzi wenu masuala ya ulipaji kodi na masuala ya rushwa," alisema 

Alisema kutokana na shule za MHL kufanya vizuri katika mitihani yao,hali hiyo,imeifanya Wilaya ya Mkuranga kujulikana.

Dk. Tindwa alipongeza uongozi wa MHL kuwasomesha bure wanafunzi wanaotoka kwenye mazingira magumu walio na vipaji na wenye kufanya vizuri katika masomo yao nae anaunga mkono jitihada hizo.

"Naunga mkono yote mnayoyafanya katika kusaidia jamii,nami nachangia milioni tatu kwa kuwaunga mkono,ambapo shilinngi milioni mbili zitumiwe kwa kusomesha wanafunzi tisa wanatoka katika mazingira magumu ambao watajiunga katika maandalizi ya kuingia kidato cha kwanza,shilingi laki nane atanunu bidhaa zinazotengenezwa na wanafunzi wa shule hiyo huku shilingi laki mbili  anamtolea mwanafunzi aliyepewa ofa ya kusoma bure kidato cha kwanza hadi cha nne kutoka na kuonyesha kipaji chake.

Hata hivyo Dk. Tindwa alitoa zawadi ya gari kwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Ujenzi kwa kusimamia vyema wanafunzi katika taaluma huku akitolea mfano mwanafunzi ambaye alishindikana katika shule mbalimbali lakini alipofika shule hapo aliweza kutulia na kufanikiwa kufanya vizuri kwenye mitihani yake ya kidato cha nne.

Mkurugenzi Mtendaji wa shule hizo za Sekondari zilizopo Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani St. Mathew's, Victory Ujenzi, Shule za Msingi na awali St.Mathew's ,Ujenzi na Mark's pamoja na Imagevosa iliyopo Ilula iringa na St.Mark's iliyopo Mbagala Jijni Dar es Salaam alisema shule zao zimesimamia dira ya elimu,malezi na usalama.

Alisema shule zao zimekuwa zikifanya vizuri katika mitihani yao kutokana na kuwaandaa watoto vizuri.

Alisema shule yao imekuwa na utaratibu wa kuinua vipaji vya watoto wao,ikiwamo kutoa punguzo la ada kwa mzazi mwenye watoto zaidi ya wawili,pia mzazi mwenye mtoto zaidi ya watatu mmoja anasoma bure,huku wanafunzi wanaofanya vizuri katika mitihani yao madarasani wapo wanaosomeshwa bure.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Ujenzi ya awali na msingi ,John Bosco anasema kuwa shule yao aibagui dini ikiwamo kutoa elimu kuanzia miaka miwili na kuendelea.

Alisema elimu ya ziada inafundishwa kwa wanafunzi wote,ambapo madarasa yamefungwa tehama ambapo wanafunzi ufundishwa kwa kutumia TV.

5