Miaka 0 hadi 8 umri muhimu wa makuzi ya mtoto unavyopuuzwa na wazazi, walezi

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 10:53 AM Aug 13 2024
Watoto wa umri wa chini ya miaka minane wakiwa kwenye mazingira magumu mtaani.
PICHA: MTANDAO
Watoto wa umri wa chini ya miaka minane wakiwa kwenye mazingira magumu mtaani.

SHIRIKA la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) katika ripoti yake ya Juni mwaka huu, inaeleza kwamba watoto karibu milioni 400 wanakabiliwa na ukatili wa kimwili na kisaikolojia nyumbani, ambapo kati yao asilimia 60 wapo chini ya umri wa miaka mitano.

Takwimu hizo zilizokusanywa kutoka katika mataifa 100 kuanzia mwaka 2010 hadi 2023 zinajumuisha aina zote za ukatili ikiwamo adhabu za kimwili na unyanyasaji wa kisaikolojia.

UNICEF inakumbusha kuwa, ukatili wa kisaikolojia unajumuisha maneno ya kubezwa, kupewa majina yanayochukiza kwenye jamii, wakati ukatili wa kimwili ni pamoja na matendo yote yanayosababisha maumivu mwilini au usumbufu, bila majeraha.

Akizungumzia kwa upande wa bara la Afrika, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Pwani, Edna Kataraiya, anabainisha kuwa robo tatu ya watoto walio chini ya miaka mitano wanaoishi Kusini mwa Jangwa la Sahara wapo kwenye hatari ya kutofikia hatua zao za ukuaji. 

Ni masuala yanayoibuka wakati wa mkutano wa tathmini ya kutekeleza Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi na Makuzi ya Maendeleo ya Awali ya Mtoto, unaofanyika Kibaha mkoani Pwani. 

Anasema takwimu zinaonyesha kwamba, dunia ina watoto milioni 250 wenye umri wa chini ya miaka mitano na robo tatu ya idadi hiyo ni sawa na asilimia 66 ya watoto hao wanapatikana Kusini mwa Jangwa la Sahara.

 Pia, Edna anasema zipo changamoto katika uwekezaji wa malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto kuanzia miaka sifuri hadi nane kutopewa uzito unaostahili badala yake msisitizo imewekwa kwenye kupunguza vifo. 

Kwa mujibu wa maelezo yake, kipindi hicho ni wakati muhimu wa kuboresha maendeleo ya binadamu na hivyo kupata mtaji bora wa rasilimali watu wenye tija kitaifa. 

Ili Programu hiyo kufikia malengo yake katika Mkoa wa Pwani, anaziagiza Halmashauri za Mkoa huo kutenga bajeti kwa ajili ya kutekeleza yaliyolengwa kufanyika kwenye maeneo yao. 

Mratibu wa masuala ya Malezi na Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknilojia, Dk. Hawa Selemani, anaeleza kwamba pamoja na serikali kuwekeza zaidi kwenye eneo hilo bado kuna vikwazo. 

"Kuna changamoto kwa watoto tunaowalenga, kuna walioko mitaani, ukatili na unyanyasaji havijaisha na hii inatufanya sasa tufikirie kuwa na mfumo wa pamoja wa kufuatilia yale tunayoyafundisha kwenye jamii," anasema. 

Kadhalika ni vyema kufuatilia kwenye vituo vya malezi ya watoto ili kupata uhakika kama wanatoa huduma kama kanuni zinavyoelekeza na kama wanaenda tofauti wapewe elimu itakayo kwa wawezeshaji kwenda sawa na malengo, anasema Dk. Hawa.  

Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Pwani, Lidya Mafole anasema kuwa, kwa sasa mkoa una vituo 730 vya malezi ya watoto na tunawafuatilia na kuhimiza kufuata taratibu na kanuni za kisheria zilizowekwa kwenye malezi yao. 

Mshiriki Uzima Justine, kutoka Taasisi ya Tuwalee Child Organization (TUCO) iliyopo Chalinze anasema kila taasisi kabla ya kutekeleza mradi ifanye utafiti kwa kukusanya takwimu kupitia viongozi wa serikali kwenye maeneo yao. 

“Zipo taasisi zinazofanya miradi ya watoto lakini bado matatizo yanaendelea kuongezeka kwa mfano suala la ukatili, hivyo kutokana na hali hii ni vyema kufikiria ni kwa nini matukio hayo yanaongezeka wakati taasisi nyingi zimejikita kwenye kutekeleza miradi? Ndipo unapokuja umuhimu wa kuanza na utafiti,” anasema Justine.

 Kadhalika anaomba Kamati za Ulinzi na Usalama kwenye wilaya kuwa na ajenda ya watoto kwenye vikao vyao zinazoanzia kwenye kamati za ngazi za tarafa, kata, vijiji na vitongoji au mtaa.

 Pia, anashauri kuzingatia idadi ya watoto kwenye vyumba vya madarasa sambamba na kutumia miongozo iliyoandaliwa na serikali itakayosaidia katika kuimarisha malezi na makuzi bora ya watoto.

 Mwakilishi wa Shirika la Tecden, Christopher Peter, akizungumzia suala la malezi ya watoto katika jamii kwenye mkutano huo, anaitaka jamii kuzingatia zaidi ulinzi, usalama, haki na mahitaji ya watoto ili wakue salama.

Programu hiyo, katika  Mkoa wa Pwani inatekelezwa na serikali kwa kushirikiana na Taasisi ya Anjita, Shirika la Tecden, Children in Crossfire na Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC)

 Peter anakumbusha kuwa, serikali inataka kila mwanaume aambatane na mwenza wake kwenda kliniki kulinda afya ya mjamzito na mtoto jambo ambalo litaleta ushirikiano chanya katika masuala ya malezi na makuzi ya mtoto.

 MAMBO YA KUZINGATIA

Washiriki wa mkutano huo wanasisitiza kuwa, ili kuwa na malezi bora katika kipindi cha miaka sufuri hadi minane katika ukuaji wa mtoto, ni muda ambao ubongo unakua kwa kasi na unachukua taarifa nyingi za mazingira mbalimbali wanapoishi.

Kwa hivyo, malezi na makuzi anayopata yanaweza kuwa na athari mbaya au bora katika maisha yake yote.

Aidha, yapo madhara ambayo yanaweza kutokea endapo mzazi au mlezi hatamzingatia mtoto ipasavyo katika kipindi hicho. Madhara hayo ni pamoja na watoto ambao hawapati vichocheo vya kutosha kiakili wanaweza kuwa na shida katika kujifunza, kutatua matatizo yanayowakabili  na kukosa kuzingatia maelekezo.

Aidha, malezi mabaya yanaweza kusababisha watoto kuwa na matatizo ya kihisia kama vile wasiwasi, unyogovu na ukosefu wa kujithamini.

Watoto ambao wanakua katika mazingira yenye ukatili au kupuuzwa wanaweza kuwa na tabia za ujeuri, utovu wa nidhamu, na uasi na wale ambao hawapati lishe bora na huduma za afya hawawezi kukua kikamilifu.

UBONGO IMARA

Pia, kipindi hicho ni muda ambao ubongo wa mtoto unaundwa, unakuwa na miunganisho mipya, kila sekunde huunda msingi wa jinsi mtoto atakavyofikiria, kujifunza na kujichanganya na wenzake.

Watoto wanahitaji kuhisi kuwa, wanapendwa na kutunzwa; na katika kipindi hiki wazazi na walezi wazungumze na watoto mara kwa mara na kuwasikiliza kwa makini huku nidhamu ikipewa kipaumbele, upendo na maonyo ya kuwaelimisha.

Pia wazazi na walezi wanapaswa kuchochea akili za watoto wao kwa kuwasoma, kucheza nao, na kuwapeleka kwenye shughuli mbalimbali za kujifunza na hiyo itaimarisha malezi mazuri kwa watoto wao kukua na kuwa watu wazima wenye afya bora na furaha.

HALI HALISI 

Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022 idadi ya watoto wenye umri sifuri  hadi miaka minane nchini ni milioni 16.6 sawa na asilimia 27 ya Watanzania Bara.

Katika idadi hiyo asilimia 47 ya watoto wenye umri kati ya miaka miwili hadi mitano wanaoishi na mama zao wanaelezwa kuwa kwenye muelekeo sahihi wa ukuaji timilifu katika maeneo ya afya kujifunza na kihisia.

 Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya utafiti wa afya ya uzazi na mtoto na viashiria vya malaria ya mwaka 2022 kutoka Ofisi ya Takwimu ya Taifa na kwamba asilimia 53 ya watoto wa umri huo wanatajwa kwamba hawako kwenye mwelekeo sahihi wa ukuaji timilifu.

 Kwa vigezo hivyo ni lazima kufanya kazi ya ziada na kubadilisha changamoto za watoto ili Tanzania inapoelekea kwenye kuandaa dira ya 2050 iwe na watoto bora kwa maendeleo ya kizazi cha sasa na kijacho.