MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imesema tangu kuanzishwa Mfumo wa Ufuatiliaji Gari (VTS-Vertical Tracking System) umedhibiti ajali zitokanazo na mwendokasi, lakini hivi sasa kuna matukio ya ajali yatokanayo na uchovu wa madereva.
Uchunguzi uliofanywa na LATRA unaonesha kwa kipindi cha Julai mwaka huu katika ajali 15 zilizotokea, nane zilitokea alfajiri na zilisababishwa na uchovu wa madereva.
Bingwa Mbobezi wa Mfumo wa Fahamu (Neurologist) kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)-Mloganzila, Dk. Henrika Kimambo, anasema kuendesha gari na uchovu ni sawa na kuendesha ukiwa umelewa.
Bingwa Mwandamizi wa Afya na Magonjwa ya Akili kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Saidi Kuganda, amesema uchovu huathiri akili na humsababishia anayeendesha chombo cha moto au mashine kukosa umakini.
Akifafanua kuhusu ajali za barabarani na mifumo mbalimbali, Ofisa Mdhibiti Ubora (Quality Assurance Officer) kutoka LATRA, Japhet Kabelege, alisema mamlaka hiyo sasa inakuja na mbinu mpya ya kufuatilia mwenendo wa dereva akiwa safarini, asiendeshe gari zaidi ya saa nane, kama ilivyo kisheria.
Kabelege aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati LATRA ilipotoa mafunzo kuhusu kanuni mpya za udhibiti wa usafiri wa nchi kavu, kwa waandishi wa habari kutoka Taasisi ya Waandishi wa Habari za Usalama Barabarani (TRSJNET) pamoja na Taasisi ya Waandishi wa Habari za Afya ya Akili (TAMHJO).
“LATRA imeimarisha matumizi ya teknolojia kwa kutumia mifumo ya kidigitali katika ukusanyaji wa taarifa na mienendo ya madereva pindi wanapokuwa barabarani, kuimarisha usalama barabarani. VTS imeanzishwa mwaka 2017 na matokeo ni chanya.
“Tunatarajia kuja na mfumo wa kamera ambao utaanza kufuatilia basi yaani idadi ya abiria hasa wanaozidi kwenye gari na yanayoendelea ndani ya gari. Kamera itapima uchovu, ujazaji wa abiria na mwenendo.
“Baadaye mabasi yote yatakuwa na kamera zipatazo tatu pande tofauti za basi, mbele, nyuma na alipo dereva.
“Hadi Julai 31 idadi ya magari yaliyosajiliwa katika mfumo wa VTS ikiwamo ya kukodiwa binafsi (special hire), mabasi ya wanafunzi na ya abiria 10,850. Kusajili gari katika mfumo huu ni lazima, ili kufuatilia gari hasa ya abiria.
“Mfumo huu husaidia kutoa taarifa kutoka kwetu kwenda kwa mkoa husika na iwapo basi linatembea kwa mwendokasi hatua zitachukuliwa mara moja.
“Ajali za Julai mwaka huu, nyingi zilizotokea hazikuzidi mwendokasi ulikuwa 77 na 83 au 67 kabla ya ajali. Asilimia kubwa sio ajali za sababu ya mwendokasi, ila uchovu na uzembe wa madereva ndio sababu kuu.
“Tulibaini basi lililotumbukia mtoni, tulipomfuatilia dereva tulibaini aliendesha zaidi ya saa 12 na abiria mmoja aliyehojiwa alisema dereva alisinzia na aliungamisha safari ndefu akielekea pia Tunduma.
“Tunakuja na mfumo wa ‘i-button’ na itakuwa takwa la lazima na kisheria mmiliki wa basi afunge mfumo huu, pamoja na VTS utakaofuatilia mwenendo wa dereva na basi lote.
“Mfumo huu utamfuatilia dereva na kumsoma dereva na baada ya saa nane italeta taarifa namna anavyoendesha akizidisha muda huo, tutajua na atakuwa amevunja sheria,” alisema Kabelege.
“Hadi Julai mwaka huu, magari 2,488 yalikuwa yamesajiliwa katika mfumo wa ‘i-button’.”
Ofisa Leseni na Usajili LATRA, Mbwana Ndaro, alisema ajali inapotokea mfumo wa VTS unaonyesha mwendokasi na eneo ilipotokea.
“Mfumo huu umesaidia ingawa wapo wachache ambao wanachezea mfumo wa VTS. Madereva 24 wamesitishiwa leseni kwa mwendokasi Julai, mwaka huu.”
ATHARI ZA UCHOVU
Dk. Kuganda amesema kufanya kazi bila kupumzika kuna athari. “Ukifanya kazi nyingi kupita uwezo wako na kwa muda mrefu utachoka mwili na akili. Kitakachofuata ni ‘burn out’...mwili umechoka na akili pia imechoka. Hii ni dalili ya kisaikolojia.
“Lakini kwa mtu ambaye hapumziki, anaona hana haja ya likizo ni mfanyakazi bora au dereva anaendesha muda mrefu hii inaweza kusababisha kuondoa umakini na kukosea kile anachokifanya kama ajali au kuharibu kazi.
“Pia anaweza kupoteza usingizi ukienda hospitali kwa daktari mzuri atakwambia ukapumzike. Na ndio maana katika utumishi wa umma, ni lazima likizo ukapumzike, ile ina maana kiafya sio ilizuka tu.”
Bingwa Bobezi wa Mfumo wa Fahamu (Neurologist) kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)-Mloganzila, Dk. Kimambo, anasema, “Mojawapo ya kazi ya ubongo ni kufanya uamuzi, kuwa makini, ufanisi, kumbukumbu. Kuwa na mwitikio wa haraka kutokana na vichocheo vilivyomo kwenye mazingira husika.
“Uchovu (fatigue) husababisha kiwango cha juu cha inflammation mwilini na mabadiliko ya homoni (ambazo huhusika katika nguvu na kuzingatia jambo).
“Hivyo basi ‘fatigue’ huathiri utendaji kazi wa ubongo na kusababisha kupungua kwa umaskini, kutofanya maamuzi sahihi kwa wakati, kuchelewa kwa mwitikio wa mwili kwa vichocheo vya nje/mazingira,” alisema bingwa huyo.
Alisema mfumo wa kumbukumbu kutofanya kazi kwa ufanisi huchangia au husababisha ajali kutokea na utafiti unaonesha, kuendesha gari ukiwa mchovu ni sawa sawa na kuendesha gari ukiwa umelewa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED