Mbowe awapa kibarua viongozi wajao

By Restuta James , Nipashe
Published at 10:25 AM Jan 22 2025
Mbowe awapa kibarua viongozi wajao.
Picha: Mtandao
Mbowe awapa kibarua viongozi wajao.

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na mgombea wa nafasi hiyo katika uchaguzi wa jana, Freeman Mbowe, amewasihi viongozi watakaoshika nyadhifa, wakijenge chama katika misingi ya maadili na nidhamu.

Akifugua mkutano wa chama hicho jana, Mbowe alisema: "Tumeona minyukano kadha wa kadha. Jambo  hili si sifa, ni aibu ya chama ambayo hatupaswi kuliendeleza. Yeyote atakayechukua kijiti cha kukiongoza chama hiki, Kamati Kuu ijayo, wajibu wa kwanza tunaowaachia warithi wa mikoba yetu ni kurejesha nidhamu, kurejesha kuheshimu maadili ya chama hiki na kuhakikisha hakuna matusi ndani ya CHADEMA," alisema.

Mbowe alisema wajibu wa viongozi wajao ni kuhakikisha kila mwana CHADEMA anamjenga mwenzake na kuimarisha chama kama taasisi.

"Ambaye atakataa kukubaliana na msimamo huu, huyo si mwenzetu. Niwashauri na kuwasihi sana, uwapo wetu leo unaakisi maumivu na jasho la watu walioumia kuijenga CHADEMA," alisema.

Alisema minyukano, kubezana na kudhalilishana haupaswi kuwa utamaduni wa CHADEMA kwa kuwa inabomoa haiba na heshima ya chama, hivyo kusisitiza kuwa wanachama, viongozi na wafuasi wa CHADEMA wana dhamana ya kukilinda chama kwa gharama yoyote. 

"Chama hiki hatutakiruhusu kwa namna yoyote eti kwa sababu pengine kura za Mbowe, Lissu au Odero hazikutosha, uchaguzi huu haupaswi kuwa vita bali  unapaswa kuwa furaha ya ujenzi wa demokrasia," alisema.

 Alisema kuna watu wanadhani CHADEMA itamaliza uchaguzi ikiwa vipande vipande, jambo ambalo alisema anaamini halitatokea bali itamaliza ikiwa imara zaidi akitumia kaulimbiu ya 'stronger together'.

 Kaulimbiu  ya ‘stronger together’ imeletwa ili kuwakumbusha wanachama kwamba pamoja na presha iliyojengwa wakati wa maandalizi ya mkutano na uchaguzi huo, wanapaswa kuendelea kuwa pamoja.

 "Katikati ya tofauti zetu, bado umoja wetu ndio nguvu yetu. Katikati ya mitazamo tofauti, bado kwa pamoja tuna nguvu...kauli hii ni kielelezo cha utayari wa Kamati Kuu kwamba pamoja na tofauti zetu tukilinde chama chetu, heshima ya chama chetu ilindwe.

"Chama hiki leo kimebeba ndoto ya taifa, sio ndoto ya Mbowe wala ndoto ya viongozi wa meza kuu. Wako Watanzania maelfu ambao hawana kadi za Chadema lakini wanaamini kesho ya watoto wao itatokana na Chadema," alisema.

 Mbowe alisema ni jukumu la wanachama na viongozi ngazi zote kulinda heshima na nguvu CHADEMA, kwa kukijenga katika maadili na nidhamu.

 Alisema chama hicho kilizaliwa Januari 21, 1993 kwa kupata usajili wa kudumu na kwamba uchaguzi unafanyika kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 32 ya uhai wake.

 Mwonekano  wa sasa wa chama hicho, alisema ni safari ya miaka 32 yenye mchanganyiko wa hisia za maumivu, jasho na damu. Alisema CHADEMA kimefanikiwa kuwa chama kikubwa ndani ya nchi kutokana na 'makamanda' walisimama imara kukilinda kwa nguvu na akili.

 "Wako wengine tulioanza nao safari hii, hawakuweza kuiona siku ya leo, nikianza kuhesabu waasisi kama wako walio hai hawazidi asilimia tano," alisema.

 Mbowe alisema chama hicho kimejengwa na wanachama wote wa CHADEMA hatua kwa hatua na kwamba sio nguvu za viongozi.

 "Ndio maana tunasema siku zote chama hiki ni mpango wa Mungu. Dhoruba na mishale tuliyopitia, leo tuko hapa kwa sababu Mungu anakusudi na chama hiki kwa sababu ya Tanzania.

 "Mtakaopewa mikoba ya chama hicho lazima mkarekebishe, inawezekana tukavumilia matusi kipindi hiki cha chaguzi lakini msingi wa CHADEMA haupaswi kuwa matusi," alisema. 

 Mbowe amesema CHADEMA itamaliza uchaguzi wakiwa wamoja na kwamba uchaguzi huo sio vita.