SERIKALI imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini ikiwemo upande wa miundombinu ya uangazi wa hali ya hewa pamoja na kuwajengea uwezo wafanyakazi wake.
Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alipozindua Mradi wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani wa “Systematic Observation Financing Facility (SOFF) - Project” katika Ukumbi wa Hotel ya Midland Inn View, Dodoma.
Majaliwa amesema lengo la Serikali la kuendelea kufanya maboresho hayo ni kuwezesha utoaji wa utabiri wa hali ya hewa na tahadhari za matukio ya hali mbaya ya hewa.
"Miongoni mwa uwekezaji huo ni ununuzi wa rada saba za hali ya hewa, upanuzi wa Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa na uboreshaji wa vifaa vya hali ya hewa kwa kuondoa vifaa vinavyotumia zebaki kwa mujibu wa matakwa ya Mkataba wa Minamata," alisema Majaliwa.
Aidha, alisema, Serikali ya Tanzania katika kuunga mkono utekelezaji wa mradi wa SOFF imetenga fedha za kununua Vituo 11 vya Hali ya Hewa. Vituo hivyo vinavyojiendesha vyenyewe vitachangia data katika Mtandao wa Kimataifa wa Uangazi.
Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali inaunga mkono kwa kutoa mchango wa zaidi ya dola za Marekani milioni nne ambazo ni thamani ya mchango kwa njia ya huduma zisizo za kifedha (In-Kind contribution). “Jitihada zote hizo, zinaonesha dhamira ya dhati ya Serikali katika kuboresha miundombinu ya hali ya hewa.”
Akizungumzia kuhusu uzinduzi wa mradi wa SOFF “SOFF - Investment Phase Project”, Majaliwa amesema mradi huo una umuhimu mkubwa siyo tu kwa kukidhi mahitaji ya data za hali ya hewa na tabianchi kwa ajili ya utabiri wa hali ya hewa duniani, bali pia kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa nchi yetu ya Tanzania.
Amesema hatua hiyo inalenga kuimarisha upatikanaji na ubadilishanaji data za hali ya hewa kimataifa, hivyo kuimarisha huduma za hali ya hewa na tahadhari za matukio ya hali mbaya ya hewa.
“Mafanikio katika utekelezaji wa SOFF yatachangia sana kuimarisha ustahimilivu wa matukio ya hali mbaya ya hewa kwa maendeleo endelevu nchini”, alisema.
Pia ameweka wazi kuwa uchumi wa nchi nyingi zinazoendelea unategemea sana sekta zinazohusiana moja kwa moja na hali ya hewa, ambazo ni kilimo, lakini pia, ufugaji, nishati, maji, afya, madini na usafirishaji.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED