Naibu Waziri wa Fedha azindua Bahati Nasibu ya Taifa

By Frank Monyo , Nipashe
Published at 05:37 PM Jan 21 2025
Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande.
Picha: Mpigapicha Wetu
Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande.

Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande, amezindua rasmi Bahati Nasibu ya Taifa Tanzania, hatua kubwa kwa sekta ya michezo ya kubahatisha nchini.

Uzinduzi huo umefanyika katika hafla ya kihistoria ambapo Chande ameeleza umuhimu wa mpango huo katika kuchochea maendeleo ya kitaifa, kuongeza ajira, na kuhamasisha ufadhili wa miradi ya kijamii.

Katika hotuba yake, Chande amesema, "Leo ni siku ya kihistoria kwa Tanzania. Kwa kushirikiana na ITHUBA kama mwendeshaji rasmi wa Bahati Nasibu ya Taifa, tunatoa kipaumbele kwa uvumbuzi, uaminifu, na uwazi. Bahati Nasibu ya Taifa itachochea ukuaji wa uchumi, kutoa ajira mpya, na kufadhili miradi ya maendeleo kwa ajili ya kuinua maisha ya wananchi wetu." amesema Chande

Amesema mpango huo, unaosimamiwa na ITHUBA, Kampuni inayoongoza barani Afrika katika kuendesha michezo ya Bahati Nasibu, unalenga kuleta mapinduzi katika sekta hiyo, kuchochea maendeleo ya kitaifa, na kutoa fursa kwa kila Mtanzania kushiriki.

Fursa za Kusisimua za Michezo kwa Wote; Bahati Nasibu ya Kitaifa itakuwa na mkusanyiko wa michezo mbalimbali ya kuvutia iliyoundwa mahsusi kwa ajili ya kuwashirikisha na kuwaburudisha Watanzania, ikiwa ni pamoja na LOTTO, TAMBA NA NAMBA, SPIN4CASH, na TOBOA CHAP CHAP. Tiketi zinaanzia bei ya Shilingi 100 tu za Kitanzania, kuhakikisha kila mtu anaweza kushiriki.

Kila tiketi itakayouzwa itachangia kuboresha michezo, elimu, na miradi ya kijamii, aliongeza Mheshimiwa Chande. Bahati Nasibu ya Taifa hii ni mfano wa jinsi michezo ya kubahatisha inavyoweza kutumika kama chombo cha maendeleo endelevu huku ikiwaletea washiriki furaha.

5

Ujumbe wa Afisa Mtendaji Mkuu wa ITHUBA Group,  Charmaine Mabuza, umesisitiza dhamira ya kampuni hiyo katika maendeleo ya Tanzania. ITHUBA inajivunia kushirikiana na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT) kuendesha Bahati Nasibu ya Taifa. "Dira yetu ni kutoa uzoefu wa hali ya juu wa michezo ya Bahati Nasibu kwa uwazi, kuburudisha, na kusaidia maendeleo endelevu. Bahati Nasibu hii si tu kuhusu michezo bali pia ni sehemu ya kuinua jamii zetu na kuwekeza katika mustakabali bora wa Tanzania."  amesema

Kwa usimamizi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), Bahati Nasibu ya Taifa itazingatia viwango vya juu vya uwazi na haki. Balozi Modest Mero, Mwenyekiti wa GBT, amebainisha umuhimu wa uadilifu katika mpango huu. "Sifa ya ITHUBA katika uwajibikaji wa kimaadili na uvumbuzi unaifanya Kampuni hii kuwa mshirika bora." amesema 

Amesema Bodi ya Michezo ya Kubahatisha itahakikisha Bahati Nasibu ya Taifa inafanya kazi kwa uwazi na uaminifu kama jukwaa salama linalochangia malengo ya kiuchumi ya Tanzania.

Bahati Nasibu ya Taifa inatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya michezo ya kubahatisha nchini. Mapato ya tiketi yatatumika kufadhili maendeleo ya michezo katika ngazi ya msingi, uwezeshaji wa vijana, na miradi muhimu ya kijamii, kuimarisha jukumu la Bahati Nasibu ya Taifa kama chombo cha maendeleo ya kijamii.

Baadhi ya Michezo inayopatikana Kupitia Bahati Nasibu ya Taifa:

Bahati Nasibu ya Taifa itatoa michezo mbalimbali ya kuvutia, ikiwa ni pamoja na:

  • LOTTO: Jakpoti kubwa za kila siku.
  • TAMBA NA NAMBA: Mchezo wa haraka unaofanyika kila baada ya dakika tano.
  • SPIN4CASH: Michezo ya papo hapo yenye malipo ya haraka.
  • TOBOA CHAP CHAP: Michezo yenye mada za kuvutia kama "MFUGA KUKU" na "TUNDA KITMATI."

Fursa kwa Wadau Wote:

Bahati Nasibu ya Taifa inatarajiwa kutoa fursa kubwa kwa wadau mbalimbali, ikiwa ni pamoja na:

  • Washiriki: Zawadi za zaidi ya dola milioni 60 zinatarajiwa kutolewa katika mwaka wa kwanza.
  • Wauzaji na Washirika wa Biashara: Kamisheni za takriban dola milioni 6.6, pamoja na mafunzo na msaada wa kimasoko.
  • Vyombo vya Habari: Bajeti ya dola milioni 3.5 imetengwa kwa masoko na matangazo.

Bahati Nasibu ya Taifa itahakikisha ushirikishwaji wa kila mmoja wetu kwa kutoa tiketi kupitia majukwaa ya kidigitali, huduma za simu, na vituo vya rejareja kote nchini. Juhudi za kufikia maeneo ya vijijini pia zimepangwa kuhakikisha kuwa hata jamii za pembezoni zinaweza kushiriki na kufaidika.