Mchinjita awakaribisha ACT, watakaoichoka CHADEMA

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:26 PM Jan 21 2025
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Tanzania Bara, Isihaka Mchinjita.
Picha: Mpigapicha Wetu
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Tanzania Bara, Isihaka Mchinjita.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Tanzania Bara, Isihaka Mchinjita, amefungua milango ya chama hicho kwa wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wanaoona kuwa safari yao ya kidemokrasia inahitaji jukwaa jipya.

Mchinjita amesema hayo kwa hoja kuwa mwenendo wa misigano na minyukano ya kisiasa miongoni mwa kambi kuu zinazowania nafasi ya kuongoza Chadema, unaweka rehani uwezo wa kufanya kazi pamoja baada ya uchaguzi.

Leo, Januari 21, 2025, Chadema inafanya uchaguzi wa kumchagua mwenyekiti wa chama hicho atakayekuwa kiongozi kwa miaka mitano ijayo. Ushindani mkubwa upo kwa Freeman Mbowe anayetetea nafasi hiyo na makamu wake Tundu Lissu. Mgombea mwingine katika nafasi hiyo ni Charles Odero.

Mshindi anatarajiwa kujulikana leo baada ya wajumbe kutoka mikoa 33 ya chama hicho kupiga kura, na sanduku la kura kuamua atakayepata asilimia 50 ya kura zote au zaidi.

Kupitia taarifa aliyoitoa leo kwenye mtandao wake wa X (zamani Twitter), Mchinjita ametuma salamu za heri kwa wanachama wa Chadema akiwataka kufanya uchaguzi kwa amani. Amesema ACT-Wazalendo imekuwa kimbilio mara zote kwa wahanga wa demokrasia nchini.

"Tunawakaribisha wote wanaoona safari yao ya kidemokrasia inahitaji jukwaa jipya. Karibuni ACT Wazalendo yenye tunu ya uongozi wa pamoja, uwazi, na mijadala ya masuala," amesema Mchinjita.