Vijana wa bilioni mbili waendelea kusota rumande

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 01:59 PM Jan 21 2025


Baadhi ya vijana hao wakiongozwa kuingia  kwenye chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Dar es Salaam huku wakiwa wameficha sura zao kusikiliza kesi inayowakibili ya Uhujumu Uchumi.
Picha: Grace Gurisha
Baadhi ya vijana hao wakiongozwa kuingia kwenye chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Dar es Salaam huku wakiwa wameficha sura zao kusikiliza kesi inayowakibili ya Uhujumu Uchumi.

Vijana sita wanaokabiliwa na mashtaka 68 ya uhujumu uchumi, yakiwemo madai ya kufanya udanganyifu kwa kutumia mashine za kielektroniki za utoaji risiti (EFD), na kuisababishia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hasara ya shilingi bilioni 2.1, wanaendelea kusota rumande kutokana na upelelezi wa kesi yao kutokukamilika.

Waliofikishwa mahakamani ni Stanslaus Mushi (27), mfanyabiashara mkazi wa Malamba Mawili, Nemence Mushi (29), Rose Nanga (33) ambaye ni mhasibu wa soko mkazi wa Kimara B, Hussein Mlezi (37) fundi wa kompyuta mkazi wa Mbagala Kuu, Edwin Mark (22) mkazi wa Yombo Vituka, na Salim Salehe (45) mchoraji.

Mashtaka yanayowakabili yanahusisha matumizi mabaya ya mashine za EFD kwa lengo la kupotosha mfumo wa TRA, pamoja na upatikanaji wa namba za utambulisho wa mlipakodi (TIN) na usajili wa Ongezeko la Thamani (VAT) kwa njia ya udanganyifu.

Wakili wa Serikali, Rhoda Maingu, akisaidiana na Wakili Auni Chilamula, aliieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni mbele ya Hakimu Mkazi Amos Rweikiza kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Hata hivyo, Wakili wa mshtakiwa wa kwanza na wa pili, Estei Madulu, alipinga hoja hiyo, akisema:

"Suala la upelelezi kutokukamilika limekuwa ni jambo la kawaida. Kwa mujibu wa haki jinai, mshtakiwa anapofikishwa mahakamani, upelelezi unapaswa kuwa umekamilika ili kesi iweze kuendelea."

Wakili Madulu aliongeza kuwa, kama upelelezi haujakamilika, ni bora kesi hiyo ihamishiwe mahakama yenye mamlaka ya kusikiliza badala ya kuendelea kuahirishwa.

Hakimu Rweikiza aliwataka mawakili wa serikali kutoa maoni yao kuhusu hoja hizo na kufafanua kuwa Hakimu Mkazi Mkuu, Radhamani Rugemalira, anayesikiliza kesi hiyo, alikuwa nje ya ofisi kwa udhuru wa kikazi. Aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 5, 2025.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka:

  1. Mashtaka ya kwanza hadi ya 64 yanawahusu washtakiwa kutenda makosa ya udanganyifu kati ya Novemba 1 na Novemba 30, 2024, kwa kutumia mashine ya EFD kwa njia inayopotosha mfumo wa TRA, mashine hiyo ikiwa mali ya Hadija Songea.
  2. Mashtaka ya 65 na 66 yanawahusu Stanslaus Mushi, Rose Nanga, na Salim Salehe kwa kupata usajili wa namba ya TIN kwa njia ya udanganyifu kati ya Juni 1 na Juni 30, 2024.
  3. Katika shtaka la 67, Mushi na Nanga wanatuhumiwa kusajili mashine ya EFD kwa jina la Hadija Songea kwa njia ya udanganyifu kati ya Juni 1 na Juni 30, 2024.
  4. Shtaka la 68 linawahusu washtakiwa wote kwa madai ya kuisababishia TRA hasara ya shilingi 2,160,310,567.51 kati ya Novemba 1 na Novemba 30, 2024.

Hakimu aliwaeleza washtakiwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi, hivyo hawapaswi kujibu mashtaka yao.

Baadhi ya washtakiwa walionekana wakijifunika nyuso zao walipoongozwa kuingia katika chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni kusikiliza kesi hiyo ambayo inazidi kusubiri kukamilika kwa upelelezi.