Wiki ya Sheria kuanza na migogoro wafugaji, ardhi

By Ashton Balaigwa , Nipashe
Published at 11:27 AM Jan 22 2025
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro
Picha: Ashton Balaigwa
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro

MAHAKAMA Kuu Tanzania Kanda ya Morogoro, kwa kushirikiana na taasisi 45 wameweka kliniki ya msaada wa kisheria bure, kwa wananchi wa mkoa hapa, katika wiki ya sheria inayozinduliwa Januari 25, mwaka huu.

Kaimu Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro, Stephen Murimi, amesema hayo wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu  maandalizi ya  maadhimisho hayo  kwenye  kanda ya  hiyo.

Kaimu Jaji huyo, amewataka  wananchi kutoka wilaya zote za mkoa huo wenye mashauri yanayohitaji msaada wa kisheria, ikiwamo migogoro ya ardhi na ile ya wakulima na wafugaji, kujitokeza kupata huduma za kisheria bure.

Amesema maadhimisho hayo yatafanyika kwenye mabanda maalumu yatakayokuwa Stendi ya Zamani ya daladala, mjini hapa.

Kaimu Jaji wa Mahakama hiyo, amesema maadhimisho hayo ni utekelezaji wa nguzo ya pili na tatu ya mpango mkakati wa mahakama wa upatikanaji wa haki kwa wote na kwa wakati.

Amesema katika wiki hiyo, wananchi watapata elimu ya msaada wa kisheria bure, pamoja na kuwajengea uwezo juu ya utatuzi wa migogoro ya wakulima na wafugaji, ili kuleta ustawi na amani hapa nchini.

Kaimu Jaji Murimi amesema kuwa, kutokana na mazingira ya kanda ya Morogoro, wananchi wanajishughulisha na kilimo na ufugaji, hivyo wanaingiliana katika shughuli zao za kiuchumi.

Amasema hali hiyo, inasababisha migogoro ya mara kwa mara, hali ambayo mahakama imeona ipo haja ya kuwasaidia wananchi kwa kuwapa elimu.

Akielezea kuhusu maadhimisho hayo, amesema  yatanguliwa na matembezi kuanzia viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro  (IJC),  hadi Stendi ya Zamani ya mabasi, ambako kutakuwa na mabanda ya maonesho, yataongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa  Kilakala.

“Tupo kwa ajili ya kujenga imani ya wananchi na ushirikishwaji wa wadau, mahakama ilitambua kuwa upatikanaji wa haki ni mchakato ambao unahusisha ushiriki wa wadau wa haki jinai au jinai,” amesema Kaimu Jaji huyo.

Amesema mwaka huu, Jaji Mkuu ametambulisha kauli mbiu inayohamasisha wadau wa haki na madai, kuhakikisha wanachangia na kushiriki katika kufanikisha azma ya serikali, kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.

Ametaja shabaha kuu ni kuwa na taifa jumuishi lenye ustawi, haki na linalojitegemea, maendeleo ya jamii na kuhifadhi mazingira na uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi.

Sharifa Athumani, mkazi wa kata ya Kichangani, alifurahishwa na uamuzi huo wa msaada wa kisheria bure, kwa kuwa wananchi wamekuwa na mashauri yanayotakiwa kupatiwa utatuzi, lakini wanashindwa kuwafikia wanasheria kutokana na ukosefu wa fedha;