Dk. Biteko apongeza mafanikio ya chuo cha CBE

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:09 PM Jan 22 2025
Naibu Waziri Mkuu, Dk.Doto Biteko.

Naibu Waziri Mkuu, Dk.Doto Biteko amepongea mafanikio ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), na kukitaka kutobweteka na mafanikio hayo na badala yake waendeleze juhudi kutoa wahitimu bora.

Aliyasema hayo jana, wakati wa maadhimisho ya miaka 60 ya kuanzishwa kwa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), yaliyofanyika kampasi kuu ya Dar es Salaam.

Alisema  vyuo vikuu na vya kati nchini vimetakiwa kuboresha mitaala yake ili kutoa wahitimu wanaokidhi mahitaji ya soko la ajira la sasa na kutumia teknolojia ya kisasa katika kujibu changamoto zinazoikabili jamii. 

Alisema serikali inavitaka vyuo hivyo kuweka mkazi wa mafunzo ya ujasiriamali ili wahitimu wake waweze kuwa na ujuzi wa biashara na kuchangia kikamilifu katika ukuaji wa uchumi na pato la taifa kupitia biashara bunifu na ajira binafsi. 

Dk.  Biteko alisema vyuo kama CBE vinawajibu wa kudumisha uhusiano wake na sekta binafsi ili waweze kufahamu soko linahitaji wahitimu wa aina gani  badala ya kujifungia na kufanya mambo binafsi. 

Dk. Biteko alisema Serikali inahimiza vyuo vya elimu ya biashara kufanya tafiti za kina  zinazosaidia kutatua changamoto za kiuchumi na kubuni suluhisho endelevu kabla ya matatizo hayajatokea kwenye jamii.

“Tumeelekeza vyuo kama CBE kuhakikisha fursa za elimu zinawafikia maakundi yote ya jamii kama wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili kujumuisha watu wote kwenye uchumi wa taifa letu,” alisema

Alimpongeza Mkuu wa chuo hicho, Profesa Edda Lwoga na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Seleman Jafo kwa kuendelea kusimamia chuo hicho na kutoa wahitimu bora wanaokidhi mahitaji ya soko.

Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, alisema kwenye awamu ijayo ya mradi wa upanuzi wa vyuo vikuu (HEET), serikali itahakikisha CBE kinaingizwa kwenye orodha ya vyuo vinavyostahili kupewa fedha.

Alisema kwa miaka 60 tangu kuanzishwa kwake chuo hicho kimekuwa chachu ya maendeleo ya biashara nchini kwa kutoa maelfu ya wahitimu ambao wamekuwa wakifanyakazi katika sekta ya umma na binafsi. 

Waziri wa Viwanda na Biashara, Selemani Jafo alisema chuo hicho kimekuwa kikiendeleza uhusiano na mataifa mbalimbali duniani kama Ujerumani Finland na China.

Alisema uhusiano huo umekuwa msaada mkubwa kwa wahadhiri wa chuo hicho kwenda kujengewa uwezo katika maeneo mbalimbali na wanafunzi kupata maarifa mbalimbali kwa kwenda kujifunza kwenye vyuo vya nchi hizo. 

“Kwenye eneo la vipimo,  viwango na kidijitali kazi kubwa inaendelea kufanywa na chuo hiki  na CBE imekuwa ni ufunguo wa biashara na takwimu ulimwenguni zinaonyesha kuwa watu wengi  na hapa nchini wamejikita kwenye biashara na wengi wamepitia chuo hiki,” alisema 

Alisema chuo hicho kimekuwa kikiwapa elimu ya ujasiriamali wafanyabiashara wadogo wadogo wa mkoa wa Dar es Salaam ambapo mpaka sasa zaidi ya wajasiriamali 3,000 wamenufaika.

Mkuu wa chuo hicho, Profesa Edda Lwoga alisema chuo kimepiga hatua katika udahili ambapo jumla ya wanafunzi 22,335 wamedahiliwa katika kampasi zake za Dar es Salaam, Mwanza, Dodoma na Mbeya

Alisema chuo kimefanikiwa kupanua program zake kutoka katika ngazi ya astashahada hadi ngazi ya Shahada za uzamili na kwamba hivi sasa chuo kinatoa jumla ya program 63 zinazojumuisha ngazi ya cheti, diploma, Shahada ya kwanza na Shahada ya Umahili.

Alisema ili kuhakikisha wanawafikia watu wengi wenye sifa stahili kwaajili ya Shahada za Umahiri, CBE imeboresha mitaala yake ambapo wameanza kutoa mafunzo ya shahada za uzamili kwa njia ya mtandao (online masters).