Robo hatua inavyochangia migogoro ya ardhi K’njaro

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 05:59 PM Jan 22 2025
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu.
Picha: Mwandishi Wetu
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu.

THAMANI ya kipande cha ardhi ya Mkoa wa Kilimanjaro, bado ni shubiri kwa baadhi ya watu, na kwa wengine ni neema! Ndivyo unavyoweza kueleza, “baada ya Mkuu wa Mkoa huo, Nurdin Babu, kushangazwa na idadi kubwa ya wananchi wenye changamoto hiyo, kupanga foleni saa 11 alfajiri katika Baraza la Ardhi na Nyumba wakitafuta haki."

Akizungumza jana katika Mji wa Moshi, kabla ya kuzindua kliniki ya sheria bila malipo na kamati ya ushauri wa kisheria ya mkoa huo, Babu, amesema anashangazwa na hali hiyo, huku akitoa rai kwa wananchi wake kushiriki kwa wingi katika kliniki hiyo, ili wapate suluhu ya changamoto mbalimbali za kisheria zinazowakabili. 

Babu amesema,“Mkoa huu changamoto kubwa ni ardhi. Ukienda hapo ofisi ya ardhi wanasema baraza; yaani mimi nikiingia mpaka nashangaa, watu saa 11 wameshajaa hapo. Yaani mtu wanagombania hata robo hatua,lakini hamuachii mwenzake. Sasa hiyo ndio Kilimanjaro. Ardhi hapa ni shughuli pevu.”

Wakili wa Serikali, Mkoa wa Kilimanjaro, Tamari Mndeme.
Kliniki hiyo ya sheria bila malipo kwa wananchi, inafanyika kwa ushirikiano baina ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), na Kamati ya Ushauri wa Kisheria ya Mkoa wa Kilimanjaro.

Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Mkoa wa Kilimanajro, Tamari Mndeme, alisema ofisi hiyo, imejipanga vyema kutoa huduma za kisheria bure kwa wananchi kupitia kliniki hiyo.

Kwa mujibu wa Wakili Tamari, huduma hizo zitatolewa katika viwanja vya stendi ya vumbi jirani na stendi kuu ya mabasi ya Moshi, kati ya tarehe 21 hadi 27 Januari mwaka huu.
Baadhi ya wajumbe waliohudhuria uzinduzi wa kliniki ya sheria bila malipo.