ISMRM yaandaa kongamano kuwanoa wataalam wa mionzi nchini

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 05:28 PM Aug 13 2024
Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya ISMRM Dk. Mary Kamuzora.
Picha: Maulid Mmbaga.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya ISMRM Dk. Mary Kamuzora.

CHAMA cha Kimataifa cha matumizi ya Mionzi Sumaku katika Tiba (ISMRM) Kanda ya Afrika, na Kamati ya Maandalizi ya Kongamano la Tanzania la Tiba ya Mishipa fahamu (Neuroradiology), wameanda kongamano la pamoja la kimataifa, linalolenga kuwaongezea uelewa wataalamu wa ndani.

Akizungumza leo mkoani Dar es Salaam Mwenyekiti wa Kamati ya ISMRM, Dk. Mary Kamuzora amesema kongamano hilo la kisayansi ambalo litahudhuriwa na madaktari bingwa 250 kutoka mataifa mbalimbali, linatarajiwa kufanyika Septemba 19 - 20, mwaka huu mkoani Dar es Salaam.

Amesema mkutano huo utatanguliwa na darasa litakalohusu kuwafundisha wataalam kuhusu teknolojia mpya za MRI kuanzia Septemba 17 hadi 18, mwaka huu ambayo imeandaliwa na mtandao wa SMARTA.

“Kutakuwa na onyesho la sanaa ya MRI ya Kiafrika ambayo italenga kuonyesha mchanganyiko wa sayansi ya kipimo hicho na utamaduni wa kiafrika na harambee kwa ajili ya kufadhili watafiti wachanga na wanafunzi ambao wapo katika taaluma hii ya MRI kuwawezesha kuhudhuria mikutano kama hiyo katika siku zijazo,” amesema Dk. Mary.

1
Ameongeza kuwa dhumuni la ISMRM ni kukuza mawasiliano, utafiti, maendeleo katika nyanja za matumizi ya mionzi sumaku katika tiba na biolojia na mada zingine zinazohusiana, pamoja na kutoa njia na nyenzo za kuendelea na elimu katika nyanja hizo.

Amesema mawakilisho kadhaa ya utafiti wa kisayansi na mada za kielimu zitawasilishwa na wasomi wa Rediolojia kutoka ulimwengu, wakiwemo wanaotoka Bara la Afrika, Asia, Marekani na Ulaya. 

Kongamano hilo limeratibiwa vyama mbalimbali ikiwemo cha Madaktari Bingwa wa Rediolojia Tanzania (TARASO), Wataalamu wa Rediolojia Tanzania (TARA), Wahandisi na Wateknolojia wa Vifaa Tiba Tanzania (AMETT), Shirikisho la Fizikia la Tiba Afrika (FAMPO), Wizara ya Afya kupitia Baraza la Wataalamu wa Rediolojia (MRIPC) na Idara ya Huduma za Uchunguzi.