REGINA NDLOVU, Gwiji wa sanaa, mijadala mitandaoni kutetea wenye ualbino

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:52 PM Aug 13 2024
Regina Ndlovu.
PICHA: MTANDAO
Regina Ndlovu.

KUFIKIA Aprili 2018, ripoti za Wadau wa Kutetea Haki za Binadamu na Vyombo vya Umoja wa Mataifa, vinataja kuwa, mauaji 200 na mashambulizi zaidi ya 500 kwa watu wenye ualbino yanaripotiwa Afrika. Ni katika mataifa 27 ya Afrika Kusini ya Jangwa la Sahara, Tanzania ikiwamo.

Yote hayo ni kutokana na imani potofu iliyoko maeneo ya Afrika kwamba viungo vya albino vinaleta utajiri, nguvu za kujamiiana na pia ni tiba ya maradhi kama VVU.

Viungo vyao hutafutwa kwa sababu kama hizo Tanzania, inaripotiwa kuwa takribani wenye ulemavu wa ngozi 75 waliuawa kati ya mwaka 2,000 hadi 2016.


Pia zipo ripoti za mauaji ya wenye ulemavu wa ngozi Afrika Kusini, ingawa uhalifu huo si mwingi kama ilivyo Malawi, Tanzania na Burundi. Februari mwaka jana, mahakama ya Afrika Kusini ilimhukumu mganga wa kienyeji kufungwa maisha kwa kumuua albino mwanamke mwenye miaka 20.

Katika kukabiliana na uhalifu huo, unaohusishwa na ushirikina, Regina Mary Ndlovu (34), raia wa Zambia anayeishi na ualbino, anaendeleza harakati mitandaoni kupinga ukatili huo.

Anasema amekuwa kwa shida katika utoto wake, kwa kuwa hakuna aliyeelewa ualbino ulikuwa nini wakati huo, alipozaliwa.

Wapo waliodhani mama yake alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Mzungu, hivyo baba yake aliwatelekeza , lakini baadaye wakapatanishwa, anasema, inaandika BBC.

Akiwa mtaani na popote watoto wengine mara nyingi walimdhihaki na kumwita majina, kana kwamba wanamwogopa.

Tabia hiyo iliendelea hata shuleni, huku hata mwalimu wake shule ya msingi akisema hastahili kuwa darasani, kutokana na matatizo ya macho, anasema.

Tatizo hilo liliendelea hadi sekondari walimu wakimrusha kwenda madarasa mengine ingawa hakujua kusoma na kuandika, kisa kumkwepa. 

Alinyanyaswa kingono na kimwili akiwa na miaka nane na rafiki wa familia yao. Kisha akiwa katika shule binafsi nchini Zambia, alinyanyaswa kiakili na kimwili na mwalimu.

Simulizi ya Regina anayeishi na ualibino, inasema, alianza kunyanyaswa kingono na rafiki wa familia yao akiwa na miaka nane na kwamba haikuwa mara ya kwanza wala ya mwisho.

Anasema mambo hayo yalifanyika Ennerdale, Afrika Kusini, na rafiki huyo wa familia alikuwa akitumia kisingizio cha kuwatembelea wazazi wa Regina na kumnyanyasa mara kwa mara miaka mingi.

Hakuwa yeye pekee, anaiambia BBC kuwa, amekuwa akikabiliwa na kushambuliwa kwa matukio yaliyokuwa ya kingono na yasiyo ya kingono kwa miaka mingi.

Regina anasema mashambulio yanamlenga kwa sababu tu alizaliwa na ualbino.

Kuwa albino kunatokana na kuathiriwa kwa michakato ya kimbaumbile ya kuzalisha melanin, ambayo hutengeneza rangi ya ngozi ya mwili.

Wanaomshambulia wana imani potofu kwamba kumbaka anayeishi na ualbino kunamzuia kupata magonjwa, Regina anaelezea, kuwa chanzo cha kumdhalilisha huko.

Anasema wazo hili ni moja ya hadithi nyingi za hatari zinazowazunguka watu wanaoishi na ualbino.

Leo baada ya miaka mingi ya kupambana na msongo wa mawazo, anabadilisha maisha yake ni mwigizaji.

Anafanya juhudi zote kutetea uelewa bora wa hali za watu wanaoishi na ualbino na kuwaona kuwa ni wa kawaida badala ya kuwafanyia uhalifu.

Regina anasema licha ya kujifunza kusoma na kuandika miaka 10 iliyopita akiwa na umri wa miaka 24, pia ameandika na kuigiza katika mchezo wake mwenyewe kuhusu ualbino na maisha aliyopitia yeye mwenyewe.
Mama huyu aliyejifungua karibuni anataka kufanikisha na kumaliza manyanyaso kwa wengine wenye ualibino, wasipitie kile alichokiona na kuteswa kwenye maisha yao.

Anapingana na kukabili hadithi zinazozunguka hali hiyo ya kuishi na ualbino.

Anasema wengine wanaamini kuwa, nywele nyeupe za albino zinaweza kuleta utajiri mkubwa, wakati wengine wakiamini dhana potofu zaidi ikiwa ni pamoja na kufanya ngono na mtu mwenye hali hiyo kunaweza kuponya magonjwa kama VVU na UKIMWI.

Kuna maelezo kuwa kuzuka kwa COVID-19, kumekuwa na uvumi wa uongo kwamba mwenye ualbino anaweza kuponya corona pia, inasema BBC.

Watu wanaoishi na ualbino wanatekwa na kuuawa kwa sababu ya imani potofu kwamba viungo vyao vya mwili vina nguvu, hata hivyo ni ushirikina na hakuna ukweli.

KUONDOKA ZAMBIA
Regina alihamia Afrika Kusini baada ya kifo cha baba yake, alipokuwa na umri wa miaka 12. Anasema wakati huo alikuwa anajidharau na kujichukia.

Anasema alijaribu mara 11 kujiua. Sasa ni msanii anaangalia harakati za kutetea watu wenye ualbino. Amefanya kazi ya uanaharakati na onyesho lake moja la wanawake, ambalo ni kuhusu Mary mwenye umri wa miaka 8 hadi mwenye miaka 25.

KUISHI UHALISIA

Regina ni mwanzilishi mwenza na mtangazaji wa kipindi cha mazungumzo ya mtandaoni, My Voice Albinism the new Era, yanayoweza kutafsiriwa kama ‘sauti yangu ualbino katika zama mpya’.
Regina anashiriki katika michezo ya kuigiza, sinema na tamthilia kunakomaanisha maana halisi au kila kitu kwenye maisha yake.

Anaonyesha maisha yake kwa sababu kupitia uigizaji wake watu wanafundishwa ukweli kuhusu ualbino. Anatumia jukwaa hilo kusimulia hadithi za kweli. Inachofanya jukwaani ni maelezo ya namna alivyonyanyaswa kwa muda mrefu pia, kupitia mateso, ubaguzi, kubezwa  na katika hali hiyo hakuwa na sauti ya kujitetea.

Regina anasema kushirikishwa katika michezo ya kuigiza, kupanda majukwaani na kuzungumzia hali ya ualbino kumemfundisha kuwa hakuna haja ya kupigana bali ni kuongeza juhudi zaidi kuwaelimisha watu kwamba mwenye kuishi na ualbino ana utu sawa na binadamu wengine.

Anahamasisha upendo na heshima kwa binadamu wote bila kujali maumbile yao.