Muhimbili-Upanga, Mloganzila kinara upandikizaji figo nchini

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:53 PM Aug 12 2024
Naibu Mkurugenzi Mtendaji MNH-Mloganzila, Dk. Julieth Magandi
Picha: Mpigapicha Wetu
Naibu Mkurugenzi Mtendaji MNH-Mloganzila, Dk. Julieth Magandi

Kwa mara nyingine Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila imefanya huduma ya Ubingwa Bobezi ya upasuaji wa kupandikiza figo kwa wagonjwa wawili ambapo figo imevunwa kutoka kwa mchangiaji kwa kutumia utaalam na njia ya kisasa ya tundu dogo (Hand Assisted Laparascopic Donor Nephrectomy), utaalam ambao unatumika Muhimbili pekee kwa hapa nchini.

Hayo yamebainishwa na Naibu Mkurugenzi Mtendaji MNH-Mloganzila, Dk. Julieth Magandi alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu huduma hiyo na kuongeza kuwa upandikizaji huo umefanywa na wataalam wa ndani kwa kushirikiana na Mtaalam mbobezi wa upasuaji wa matundu madogo kutoka Korea Kusini Prof. Park Kwan Tae 

“Upandikizaji huu umefanywa mwishoni mwa mwezi Julai, wale waliopandikizwa figo waliruhusiwa ndani ya wiki moja kutokana na afya zao kuimarika, upandikizaji huu umewezekana kutokana na uwekezaji uliofanywa na Serikali ya wamu ya sita ambao umehusisha kusomesha wataalam, kununua vifaa tiba, dawa na vitendanishi pamoja na kuweka mazingira wezeshi na rafiki ya kutoa huduma hii hospitalini hapa” ameongeza Dkt. Magandi

Aidha, Dk. Magandi ameishauri jamii kujitokeza kuwachangia ndugu zao figo kwakuwa kufanya hivyo kutawapunguzia gharama za uchujaji damu, muda wanaoutumia kupata huduma za kuchuja damu ambao wakati mwingine huchukua takribani masaa matatu kuchuja damu kwa wakati mmoja na pia kuwawezesha kurudi katika majukumu yao na hivyo kuzisaidia jamii wanazotokea.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo Dk. Immaculate Goima amesema miongoni sababu zinazosababisha magonjwa sugu ya figo ni pamoja na unywaji pombe uliokithiri, uvutaji wa sigara, matumizi holela ya dawa za kutuliza maumivu, shinikizo la damu na unywaji holela wa dawa za kienyeji.

Kutokana na upandikizaji huu unaifanya Muhimbili Mloganzaila kufikisha idadi ya wagonjwa 10 na kufanya idadi ya wagonjwa wote walipandikizwa figo kufikia takribani 102 kwa Hospitali ya Taifa Muhimbili Upanga na Mloganzila tangu huduma hizo zilipoanza MNH mwaka 2017 na kuifanya hospitali hiyo kuwa ndio hospitali pekee iliyopandikiza wagonjwa wengi figo hapa nchini.

5