Wagonjwa 102 wapandikizwa figo Muhimbili

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 09:40 AM Aug 13 2024
Timu ya Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Mfumo wa Mkojo na Figo kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)-Mloganzila, wakiendelea na upandikizaji figo kwa mgonjwa ambaye figo yake imeshindwa kufanya kazi.
PICHA: MNH-Mloganzila
Timu ya Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Mfumo wa Mkojo na Figo kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)-Mloganzila, wakiendelea na upandikizaji figo kwa mgonjwa ambaye figo yake imeshindwa kufanya kazi.

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) Upanga na Mloganzila imefanya upandikizaji figo kwa wagonjwa 102 tangu kuanza kwa huduma hiyo mwaka 2017.

Naibu Mkurugenzi Mtendaji MNH-Mloganzila, Dk. Julieth Magandi, aliyasema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu upandikizaji huo unaifanya Mloganzila kufikisha idadi ya wagonjwa 10 kati ya hao.

"Idadi ya wagonjwa wote waliopandikizwa figo inafikia 102 kwa MNH-Upanga na Mloganzila tangu huduma hizo zilipoanza mwaka 2017. Kunaifanya hospitali hii kuwa ndio pekee iliyopandikiza wagonjwa wengi wa figo nchini," alisema Dk. Magandi.

Alisema kuwa kwa mara nyingine MNH-Mloganzila imefanya huduma ya kibingwa na bobezi ya upasuaji kupandikiza figo kwa wagonjwa wawili huku figo ikivunwa kutoka kwa mchangiaji kwa kutumia njia ya kisasa ya tundu dogo (Hand Assisted Laparascopic Donor Nephrectomy).

Dk. Magandi alisema huduma hiyo imefanywa na wataalamu wa ndani kwa kushirikiana na Mtaalamu Mbobezi wa Upasuaji wa Matundu Madogo kutoka Korea Kusini, Prof. Park Kwan Tae.

"Upandikizaji huu ulifanywa mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu, wale waliopandikizwa figo waliruhusiwa ndani ya wiki moja kutokana na afya zao kuimarika, upandikizaji huu umewezekana kutokana na uwekezaji uliofanywa.

"Umehusisha kusomesha wataalamu, kununua vifaa tiba, dawa na vitendanishi pamoja na kuweka mazingira wezeshi na rafiki ya kutoa huduma hii hospitalini hapa," alisema Dk. Magandi.

Alitoa wito kwa umma kujitokeza kuchangia ndugu zao figo na kwa kufanya hivyo kutawapunguzia gharama za uchujaji damu na muda wanaoutumia kupata huduma za kuchuja damu ambao huchukua takribani saa tatu kwa mgonjwa mmoja.

Bingwa wa Magonjwa ya Figo hospitalini huko, Dk. Immaculate Goima, alisema miongoni mwa sababu za magonjwa sugu ya figo ni unywaji pombe uliokithiri, uvutaji sigara, matumizi holela ya dawa za kutuliza maumivu, presha na unywaji holela wa dawa za kienyeji.