Azam: Hatutafuti ushindi Morocco

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 09:38 AM Jul 24 2024
news
Picha: Mtandao
Kocha Msaidizi wa Azam FC, Youssouph Dabo.

BAADA ya kucheza mchezo mmoja wa kirafiki nchini Morocco wakiwa kwenye kambi ya maandalizi kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu na michuano ya kimataifa, Kocha Msaidizi wa Azam FC, Youssouph Dabo, amesema kwenye michezo hiyo hawaangalii matokeo bali kile wanachowafundisha wachezaji wao kama wamekishika.

Azam juzi ilicheza na Union Yacoub El Mansour inayoshiriki Ligi Daraja la Tatu nchini humo na kuibuka na ushindi wa mabao 3-0.

Akizungumza na gazeti hili jana, Dabo, alisema bado wanaendelea na maandalizi yao na kwa kiasi kikubwa wachezaji wake wanafuata kile wanachowaelekeza kwenye mazoezi yao.

Alisema kambi ya timu hiyo ni kwa ajili ya kuandaa timu kwa kuwapa mbinu mbalimbali pamoja na kutengeneza muunganiko mzuri kwenye kikosi, hivyo hawaangalii sana matokeo wanayoyapata.

"Tunataka kuona kile tunachowapa kwenye mazoezi wanakishika na kukifanyia kazi kwenye mechi, tunashukuru taratibu wachezaji wanachukua tunachowapa, tunaangalia namna wanavyocheza, hii kambi itatusaidia sana," alisema Dabo.

Alisema wanataka kucheza angalau mechi tatu kabla ya kurejea nchini kwa ajili ya mchezo wao wa Ngao ya Jamii dhidi ya Coastal Union utakaochezwa Agosti 8, mwaka huu kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Mshindi kwenye mchezo huo atacheza na timu itakayoshinda kati ya Simba na Yanga ambao wenyewe utachezwa siku hiyo hiyo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.