Kongole Waziri Silaa kwa kuiweza Wizara ya Ardhi

Nipashe
Published at 07:41 AM Jul 05 2024
Waziri wa Ardhi Jerry  Silaa.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Ardhi Jerry Silaa.

UUZAJI viwanja holela kutoka kwa kampuni zinazonunua ardhi na kuwapimia wananchi, umewaingizia baadhi ya wanaonunua viwanja hivyo usumbufu mkubwa.

Kampuni hizo hutoa matangazo ya kuuza viwanja ambavyo mnunuzi huahidiwa kuwa na hati.

Kwa matangazo hayo wananchi wengi hushawishika kwenda kununua, lakini wakishalipa pesa, usumbufu huanza kutokana na kutopata hati walizoahidiwa na badala yake huanza kuhangaika kuzipata.

Hivi karibuni, Wizara ya Ardhi kupitia waziri wake, ilipiga marufuku matangazo yote ya kuuza viwanja bila kupata kibali kutoka wizara hiyo mpaka ivihakiki na kuruhusiwa.

Hiyo imetokana na baadhi ya viwanja hivyo kutoendana na vipimo vinavyotakiwa kisheria.

Ukipita barabara kuu nyingi jijini Dar es Salaam, utakutana na vipaza sauti vilivyowekwa barabarani vikitangaza ofa za viwanja.

Uuzaji huu holela wa kutumia vipaza sauti ambavyo muda wote vinapiga kelele barabarani pia ni uchafuzi wa mazingira kwa njia ya kelele.

Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), linapiga marufuku kelele katika maeneo ya umma kwa kuwa ni moja ya uchafuzi wa mazingira.

Hivyo, watu hao pia wanatakiwa wachukuliwe hatua kwa kubugudhi watu wengine.

Katika kudhibiti migogoro ya ardhi huko mkoani Pwani, serikali imezuia uuzaji wa maeneo katika Kitongoji cha Mbala, Kijiji cha Chamakweza Halmashauri ya Chalinze kutoa nafasi ya kupata mwafaka wa mmiliki halali wa eneo hilo ambalo lina mgogoro wa zaidi ya miaka 20 kati ya wakulima na wafugaji.

Amri ya kusitisha uuzaji wa maeneo hayo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge kwenye ziara ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa, alipofika kusikiliza wananchi hao.

Kunenge alifikia kutoa amri hiyo kutokana na mgogoro huo huku kila upande ukidai ndio wakazi halali wa eneo hilo na kila upande ukimtuhumu mwingine kuwa mvamizi na kuuza maeneo kiholela.

Waziri Silaa aliahidi kutuma timu ya wataalamu kutoka wizarani kwa ajili ya kuhakiki mipaka ya vijiji na kutambua wakazi halali kijiji hicho. 

"Nitaunda timu ya wataalamu kutoka wizarani kufanya uhakiki wa yaliyosemwa hapa tutafanya maamuzi ambayo hayataleta taharuki, tutakapofikia mwafaka tutatengeneza mpango wa matumizi bora ya ardhi na hii itasaidia kutatua migogoro inayotolewa.”

Alielekeza viongozi wa vijiji kuzingatia Sheria namba tano ya Ardhi ambayo inatoa mamlaka ya ardhi kutolewa kwa kuzingatia taratibu zilizopo ikiwamo mikutano ya wananchi kwenye maeneo husika.

Wakati huo huo, Waziri Silaa amesema wizara yake imegawa Mkoa wa Pwani katika mikoa miwili ili kurahisisha utatuzi wa migogoro iliyopo kwa muda mrefu.

Wizara ya Ardhi, kupitia waziri wake pia imefanikiwa kutatua migogoro mingi ya ardhi kupitia kliniki zake ilizoanzisha katika wilaya mbalimbali.

Wananchi wengi ambao walikuwa wakisumbuka kupata hati, kupitia kliniki hizo wamefanikiwa kuzipata na waliokuwa na migogoro wamesuluhishwa na sasa wanaishi kwa amani.

Wizara nyingine zinapaswa kuiga mfano wa Wizara ya Ardhi ili kutatua matatizo yanayowakabili wananchi.

Waziri wa Ardhi alikuwa mstari wa mbele kusimamia kliniki hizo na kuhakikisha wananchi wanapata haki zao bila usumbufu.