TCU yaongeza siku 6 udahili vyuo vikuu

By Renatha Msungu , Nipashe
Published at 07:35 AM Oct 05 2024
Katibu Mtendaji wa TCU, Prof. Charles Kihampa
Picha: Mtandao
Katibu Mtendaji wa TCU, Prof. Charles Kihampa

TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imetangaza awamu ya tatu na mwisho ya dirisha la udahili wa wanafunzi wa shahada ya kwanza vyuo vya elimu ya juu nchini utakaofanyika kwa siku sita.

Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu Mtendaji wa TCU, Prof. Charles Kihampa, alisema dirisha hilo lilifunguliwa kuanzia jana na litafungwa Oktoba 9, mwaka huu.

Prof. Kihampa alisema wanafunzi waliochaguliwa katika awamu ya pili ya udahili, wanatakiwa kujithibitisha katika vyuo walivyochaguliwa ifikapo Oktoba 21 mwaka huu.

Alisema baada ya kukamilika kwa awamu zote mbili, tume hiyo ilipokea maombi ya kuongeza muda kutoka kwa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu (TAHILISO) kuwa wapewe muda wa kuendelea na kudahili.

“Kuna waombaji ambao hawakupata nafasi ya kudahiliwa au kutuma maombi katika awamu ya pili kutokana na sababu mbalimbali, sasa wanapaswa kutumia nafasi hii kutuma maombi katika vyuo hivyo. Hii ni nafasi ya mwisho,” alisema Prof. Kihampa.
 
 Alisema tayari TCU imeelekeza vyuo kutangaza programu ambazo bado zina nafasi na kuwataka waombaji kuzingatia utaratibu wa awamu ya tatu kama ulivyoainishwa.

Prof. Kihampa alisema waombaji waliodahiliwa katika chuo zaidi ya kimoja katika awamu ya pili na wale ambao hawakuweza kuthibitisha katika awamu ya kwanza, wanapaswa kuthibitisha udahili wao katika chuo
 kimoja kuanzia jana hadi Oktoba 21 mwaka huu. 

“Uthibitisho huo ufanyike kwa kutumia namba maalum ya siri iliyotumwa kwa ujumbe mfupi kupitia namba za simu au barua pepe walizotumia katika udahili,” alisema Prof. Kihampa.

Pia alisisitiza uthibitisho wa udahili ufanyike kupitia akaunti ambayo mwombaji aliitumia wakati wa kuomba udahili wa kujiunga na vyuo vya elimu ya juu.

Alisema kwa ambao hawatapata kwa wakati ujumbe huo, wanashauriwa kuingia katika mifumo ya udahili ya vyuo walivyodahiliwa ili kuuomba kumwezesha  kuthibitisha katika chuo husika.

Prof. Kihampa alisema kwa wale ambao watapata changamoto katika kuthibitisha tayari vyuo vyote vimeelekezwa kupokea taarifa zao, ikiwamo kuzitafutia ufumbuzi wa haraka kwa kuzingatia miongozo na
 taratizu zote zilizowekwa.

Alisema vyuo vinatakiwa kuwasilisha TCU majina ya waliodahiliwa katika awamu ya tatu kuanzia Oktoba 13 hadi Oktoba 15, mwaka huu, na Oktoba 19 vyuo vinatakiwa kutangaza majina ya waliodahiliwa katika awamu ya tatu.