KAMATI ya Utendaji ya Chama cha Mpira wa Miguu cha Wanawake Tanzania (TWFA), inatarajia kukutana leo ili kufanya uteuzi wa Katibu Mkuu mpya wa chama hicho, imeelezwa, jijini Dar es Salaam jana.
Nafasi ya Katibu Mkuu wa TWFA ilikuwa inashikiliwa na Somoe Ng'itu, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti mpya wa chama hicho baada ya kumshinda Amina Karuma.
Akizungumza na gazeti hili jana, Somoe, alisema maandalizi ya kikao hicho yamekamilika na uteuzi huo unafanyika kwa mujibu wa matakwa ya katiba ya TWFA.
"Kikao kitafanyika kesho (leo), na hili linatekelezwa kwa kufuata katiba ambayo inaelekeza Makamu Mwenyekiti anateuliwa lakini anapata baraka za wajumbe wa mkutano mkuu wa TWFA kama ambavyo ilifanyika kule mkoani Kilimanjaro.
Kesho (leo), tunakwenda kufanya uteuzi ambao baraka zake zinatolewa na Kamati ya Utendaji, ninaamini wajumbe watatimiza majukumu yao katika kulikamilisha jambo hili," Somoe alisema.
Katika uchaguzi mkuu wa TWFA uliofanyika Septemba 14, mwaka huu, nafasi ya Makamu Mwenyekiti ilikwenda kwa Beatrice Mgaya kutoka Tanga, Zena Chande wa Dar es Salaam alifanikiwa kutetea nafasi yake ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF.
Waliochaguliwa kuwa wajumbe wa Kamati ya Utendaji ni pamoja na Ndinagwe Sungura wa Rukwa, Irene Ishengoma (Dar es Salaam) na Hamisa Katambi kutoka mkoani Shinyanga.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED