Ado: ACT Wazalendo tupo kuungana na vyama makini vya upinzani

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:40 PM Oct 04 2024
Katibu Mkuu ACT Wazalendo, Ado Shaibu
Picha: Mpigapicha Wetu
Katibu Mkuu ACT Wazalendo, Ado Shaibu

Katibu Mkuu ACT Wazalendo, Ado Shaibu ametoa rai kwa CHADEMA na vyama vingine makini vya upinzani kuungana kupigania mazingira ya kidemokrasia ikiwemo Katiba Mpya, Tume Huru ya Uchaguzi, mageuzi ya Jeshi la Polisi na uhuru wa vyama vya siasa kufanya shughuli zake.

 Amesema kuwa chama cha ACT Wazalendo kipo tayari kushirikiana ili kuhakikisha CCM inaondoka madarakani.

"Sisi tuna itikadi, falsafa na sera tofauti, tuna mikakati tofauti, sisi tunachuana katika kinyang'anyilo cha madaraka au sio. Tukienda hapo sisi ni vyama  tofauti lakini ukweli ni kwamba ni muhimu sana kwa vyama vya upinzani, vyama makini vya upinzani kama tunataka kuidondosha CCM, kama tunataka kuimaliza mapema CCM ni lazima sisi tushirikiane vyama vya upinzani"

Katibu Mkuu huyo amefafanua kuwa maeneo ya kuanzia kwa vyama vya upinzani kuungana na kushirikiana, katika kufafanua amesema;

"Ni lazima tushikamane kupigania Katiba mpya, Katiba mpya sio ajenda ya chama kimoja cha siasa ni lazima tushikamane, tushikamane tupiganie Tume Huru ya uchaguzi, ni lazima tushikamane kupigania mageuzi katika uendeshaji wa Jeshi la Polisi na vyombo vya Ulinzi na Usalama, ni lazima tushikamane. Ni lazima tushikane kupigania uhuru wa kisiasa za Tanzania"

Katika kusisitiza azma hiyo Kiongozi huyo amesema kuwa chama hicho kipo tayari kuungana.

"ACT Wazalendo tupo teyari kufanya kazi na chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) na vyama vingine vya upinzani ambavyo ni makini katika agenda hizi za kupigania demokrasia ya Tanzania. 

Kauli hiyo ameitoa akihitimisha ziara ya kuyafikia majimbo 214 ya Tanzania Bara jimboni Muleba Kusini Mkoani Kagera, Jana Septemba 3, 2024.