SMZ yazuia matumizi ya mawe katika ujenzi

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 07:51 AM Oct 05 2024
Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Hassan Shaibu Kaduara.
Picha:Mtandao
Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Hassan Shaibu Kaduara.

SERIKALI ya Zanzibar imezuia matumizi na usafirishaji wa mawe katika shughuli za ujenzi kwa sababu mbalimbali ikiwamo ya hali ya mazingira.

Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Hassan Shaibu Kaduara, alisema hayo jana  wakati akizungumza na waandishi wa habari huko ofisini kwake Maisara visiwani Zanzibar.

Alisema uamuzi huo umefikiwa kutokana na uharibifu wa mazingira unaoendelea serikali ikaamuwa kupiga marufuku juu ya matumizi ya rasilimali hiyo.

Waziri Kaduara alisema kuwa katazo hilo limeangalia maslahi mapana ya taifa hivyo kila mwananchi anatakiwa kufahamu kuwa athari za kimazingira ni kubwa kuliko faida inayopatikana katika rasilimali hiyo.

"Serikali imekuwa ikipokea  malalamiko mengi kutoka kwa  wananchi juu ya athari za kimazingira juu ya rasilimali ya mawe inavyo athiri mazingira,” alisema Kaduara.

Alisema katika kipindi hiki cha katazo, ni vyema wananchi kutumia matofali kwa ajili ya msingi na utafiti uliyofanywa kutumia matofali ni rahisi kuliko kutumia mawe kwa ajili ya kujengea.

Waziri huyo alisema kuwa viwanda vinavyojishughulisha na uzalishaji wa kokoto kufanya shughuli zao katika maeneo yenye mawe ili kuendelea kutoa huduma za kokoto kwa wananchi wa visiwa wa vya Zanzibar.

Serikali, alisema imefikia uamuzi huo kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira pamoja na kuharibiwa kwa maeneo ya wananchi na serikali kwa kuzuia mawe.

Alisema serikali imekuwa ikipokea malalamiko  kutoka kwa wananchi juu ya athari wanazozipata kutokana na uwepo wa viwanda vya kusagia mawe katika maeneo ya makazi.

"Kumekuwa na malamamiko mengi wananchi wakiyatoa juu ya kuwepo mitani viwanda hivyo na sisi kama serikali tukaono kufanya uwamuzi huo," alisema Kaduara.

Alisema kuendelea kuwapo mitaani kwa viwanda hivyo ni moja ya kuondosha hata haiba ya Zanzibar kwa vile visiwa hicho ni maarufu katika shughuli za utalii.