MOI kuhudumia wagonjwa wa nje 3,000

By Mary Geofrey , Nipashe
Published at 07:05 AM Oct 05 2024
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk. Lemeri Mchome
Picha:Mtandao
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk. Lemeri Mchome

TAASISI ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI) inatarajia kuanza kuhudumia wagonjwa wa nje 1,500 hadi 3,000 kwa siku.

Hatua hiyo ni baada ya kukamilika kwa miradi mikubwa mitatu ya ujenzi wa jengo jipya ya Wagonjwa wa Nje (OPD), kukarabati jengo la Hospitali ya Tumaini na ujenzi wa Kituo cha Utengamao Mbweni.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk. Lemeri Mchome, aliyasema hayo juzi katika Kikao cha Tano cha Baraza la Tano la Wafanyakazi wa MOI, kinachoendelea jijini Dar es Salaam.

Dk. Mchome alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa mipango ya serikali kupitia Wizara ya Afya wa kuhakikisha inapunguza msongamano wa wagonjwa na kuboresha huduma kwa wananchi.

Alisema miradi hiyo itaongeza idadi ya wagonjwa watakaolazwa kutoka 362 hadi kufikia zaidi ya 500 kwa siku na kuwezesha wananchi kupata huduma bora kwa wakati.

Akifungua kikao hicho, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini MOI, Prof. Charles Mkonyi, aliwataka watumishi kuongeza ubunifu katika kutoa matibabu ili wagonjwa waweze kupona haraka na kurejea katika shughuli zao za kawaida.

“Ni lazima jamii ifahamu kuwa MOI inatoa matibabu ya kipekee kabisa tofauti na maeneo mengine, huduma zake ni za kipekee na zinahitaji ubunifu zaidi ili kuwawezesha wagonjwa kupona haraka.

“Wakati menejimenti wakiendelea na uboreshaji wa maslahi ya watumishi na miundombinu ya kufanyia kazi, niwaombe watumishi endeleeni kuwa mstari wa mbele kupiga vita rushwa, sijasikia kwa siku za hivi karibuni na ndiyo maana ninasema endeleeni hivyo,” alisema.